Mshambuliaji Mpya wa Simba John Bocco, ‘Adebayor’ amesema chini ya kocha Joseph Omog, anamatumaini makubwa ya kufanya vizuri na kuipa mafanikio timu hiyo.
Kwa mara ya kwanza tangu afukuzwe kwenye kikosi cha Azam miaka miwili iliyopita, Omog, alikutana na Bocco, na kumfundisha mbinu kadhaa za kutumia ili aweze kufanya vizuri kwenye msimu unaotarajia kuanza hivi karibuni.
Bocco amekiambia chanzo chetu kuwa anajisikia faraja kufanya kazi kwa mara nyingine na kocha Omog, kwa sababu ni kocha anayemjua vizuri na anaamini msimu ujao utakuwa na mafanikio kwake na timu ya Simba.
“Nakumbuka msimu wa kwanza kufanya kazi na Omog tulichukua ubingwa wa Ligi Kuu pale Azam na ninaamini hata msimu ujao nikiwa hapa Simba chini ya Omog tutafanya vizuri na kutwaa ubingwa,” alisema Bocco.
Mshambuliaji huyo aliyekabidhiwa jezi namba 22, amesema yeye pamona na wachezaji wenzake wamejipanga kurudisha mafanikio ya Simba ambayo yamepotea siku za karibuni na kwa ari waliyokuwa nayo hakuna kitakachoshindikana.
Amesema wanatambua nini ambacho mashabiki na viongozi wao wanakihitaji msimu ujao hivyo wanajifua kuhakikisha wanakata kiu yao kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kufanya vizuri kwenye michuano mingine watakayoshiriki mwakani.
Bocco ni mmoja wa wachezaji wanne waliosajiliwa na Simba kutoka kikosi cha Azam wengine ni Shomari Kapombe kipa Aishi Manula na Erasto Nyoni.
No comments:
Post a Comment