Habari kutoka ndani ya Simba SC zimesema kwamba, Dhaira ameanza ‘kuleta maringo’ baada ya kuona hana upinzani katika timu hiyo- kutokana na kuamini Ntalla haaminiki katika klabu hiyo na Abuu Hashimu kipa wa tatu bado mchanga kabisa.
Anarudishishwa? Juma Kaseja anaweza kurejeshwa Simba SC baada ya Abbel Dhaira kuanza kutikisa kiberiti |
Abbel aliyesaini Mkataba wa mwaka mmoja wakati anatua Simba SC Januari mwaka huu kwa kiasi kikubwa ameushitua uongozi wa klabu hiyo na sasa unataka kuchukua tahadhari dhidi yake.
Habari zaidi zinasema kwamba, wakati Mkataba wake unakaribia kumalizika, ili kuongeza Mkataba mpya, kipa huyo wa timu ya taifa ya Uganda, ameomba fedha nyingi ambazo Simba SC haiko tayari kutoa.
Na kwa kuhofia huenda anaweza akashikilia msimamo wake huo kwa kujua Simba SC haina kipa wa kuaminika zaidi yake kwa sasa, uongozi sasa unafikiria kumrejesha Kaseja.
Kaseja alitemwa mwishoni mwa msimu kwa madai ameshuka kiwango, baada ya kuitumikia klabu hiyo tangu mwaka 2003 alipojiunga nayo akitokea Moro United ya Morogoro. Mwaka 2009 alikwenda kuidakia Yanga SC kwa msimu mmoja na kurejea Msimbazi alipomaliza Mkataba wake.
Pamoja na kuachwa kabla ya dirisha la usajili kufungwa, Kaseja hakujiunga na timu nyingine yoyote zaidi ya kufanya mazoezi na timu kadhaa, ikiwemo Mtibwa Sugar na Ashanti United ili kujiweka fiti.
Katika kutengeneza hoja za kumrejesha Kaseja, Simba SC wanasema kipa huyo bado imara na msimu uliopita aliathiriwa na safu butu ya ulinzi na kukosa kocha bora wa kumnoa.
Kwa sababu hiyo, baada ya kupata mabeki bora kama Mganda Joseph Owino na Mrundi Kaze Gilbert, Simba SC inaamini Kaseja akirejea na kuongezewa kocha mzuri wa kumnoa, atarejesha makali yake.
Bwana Mapooz; Dhaira amewashitua Simba SC na sasa wanataka kumrejesha Kaseja |
Kocha wa sasa wa makipa Simba SC ni James Kisaka, lakini tayari uongozi wa klabu hiyo umekwishaanza mazungumzo na kipa wake nyota wa zamani, Iddi Pazi ‘Father’ arejee kuwanoa walinda mlango wa timu hiyo.
Habari zaidi zinasema, kuna uwezekano Kaseja akaingia kambini Simba SC mapema tu hivi karibuni hata kabla ya usajili wa dirisha dogo Januari, ili kuanza kuzoeana na wachezaji wapya waliosajiliwa timu hiyo baada ya yeye kutemwa.
Miongoni mwa wachezaji ambao walipishana milango na Kaseja Simba ni mabeki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Kaze Gilbet, viungo Twaha Ibrahim ‘Messi’, Sino Augustino na washambuliaji Zahor Pazi, Betram Mombeki na Amisi Tambwe.
SOURCE; BIN ZUBERY
No comments:
Post a Comment