tuwasiliane

Saturday, September 14, 2013

OKWI AJIUNGA NA URA KUSUBIRI HATMA YAKE KWA WAARABU - FIFA YAWAPA ETOILE MPAKA MWISHO MWA MWEZI HUU KUWALIPA MIL 480 SIMBA

 
STRAIKA wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi amejiunga na URA ya Uganda ili kujiweka fiti akisubiri hatma yake kwenye klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.
Okwi amegoma kuichezea Etoile du Sahel mpaka itakapommalizia malipo yake ya kusaini mkataba pamoja na kumlipa malimbikizo ya mishahara ya miezi mitatu.
“Nimetulia kwanza nione suala langu linaendaje na suluhisho ni nini. Ninataka sana kurudi uwanjani kucheza soka la ushindani,” alisema Okwi.
“Ishu ni kwamba hawajanimalizia pesa ya kusaini mkataba pamoja na mishahara yangu ya miezi mitatu sasa,” alisema Okwi ambaye anaendelea kujinoa na URA ingawa haruhusiwi kucheza mechi ya mashindano kwa sababu ana mkataba wa miaka mitatu na Etoile du Sahel.
Wakala wa mchezaji huyo amesema kwamba wanaendelea na mazungumzo na Etoile ili kutatua suala la Okwi ingawa habari za ndani zinasema kwamba anafanya mpango wa kumpeleka kwa mkopo kwenye klabu moja ya Daraja la Kwanza Ulaya.
Okwi aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uganda na kucheza dhidi ya Senegal wiki iliyopita katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia na kushuhudia kikosi cha Kocha Sredojevic Milutin ‘Micho’ kikiambuliwa kipigo cha bao 1-0.
Wakati Okwi akiwa na malumbano hayo na klabu hiyo ya Tunisia, Simba ambayo ilimuuza nayo inasubiri malipo ya Sh480 milioni kutoka kwa Etoile du Sahel ambayo iliahidi kulipa fedha hizo kabla ya mwisho wa mwezi huu.
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limetoa mpaka mwisho wa mwezi huu Simba iwe imelipwa.
SOURCE: MWANASPOTI

No comments:

Post a Comment