LIGI
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara imeendelea leo kwenye viwanja tofauti,
huku mabingwa watetezi, Yanga SC wakilazimishwa sare ya 1-1 na wenyeji
Mbeya City na Simba SC wakishinda 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, wakati Azam
FC imetoa sare ya 1-1 na wenyeji Kagera Sugar.
Uwanja
wa Sokoine mjini Mbeya, mabingwa watetezi walilazimika kusubiri hadi
dakika ya 82 kujihakikishia japo kupata pointi moja mbele ya Mbeya City.
Mbeya
inayofundishwa na Juma Mwambusi, ndiyo walioanza mchezo huo kwa kasi
wakishambulia zaidi kutokea pembeni na kulitia misukosuko lango la Yanga
SC.
Mbeya
inayofundishwa na Juma Mwambusi, ndiyo walioanza mchezo huo kwa kasi
wakishambulia zaidi kutokea pembeni na kulitia misukosuko lango la Yanga
SC.
Pamoja
na kocha Mholanzi, Ernie Brandts kuanzisha washambuliaji watatu, Didier
Kavumbangu, Hussein Javu na Said Bahanuzi, lakini kuzidiwa kwa timu yao
katika safu ya kiungo kuliwafanya wasiwe na madhara.
Hata
hivyo, hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake
na kipindi cha pili, Mbeya waliingia kwa kasi zaidi na kufanikiwa
kupata bao dakika ya nne tu tangu kuanza kipindi hicho.
Krosi
maridadi ya Hassan Mwasapili kutoka wingi ya kushoto iliunganishwa
vizuri kwa kichwa na Mwagane Yeya ‘Morgan’ na kumpita kipa Ally Mustafa
‘Barthez’ kama amesimama.
Baada
ya bao hilo, Yanga walicharuka na kuanza kucheza kwa nguvu na
kushambulia zaidi na almanusra mchezo uingie dosari dakika ya 58, baada
ya Didier Kavumbangu kuuwahi mpira aliokuwa akiuchezea kipa wa Mbeya
City, David Burhan na kuutumbukzia nyavuni, lakini refa akakataa bao.
Kipa
huyo alidaka shuti la Nizar Khalfan na kuanza kuuchezea mpira kwa
madaha akiudundaduna huku ameinama, ndipo Kavumbangu akamsogelea na kwa
mchecheto mpira ukamtoka kipa huyo mikononi na mshambuliaji huyo wa
Yanga akawahi kuusukumia nyavuni.
Baada ya refa Andrew Shamba kukataa bao hilo, wachezaji wa Yanga walimtia kashikashi kidogo, kabla ya kuendelea na mchezo.
Timu
ziliendelea kushambuliana kwa zamu, lakini mabadiliko yaliyofanywa na
kocha Brandts kuwaingiza mfululizo Jerry Tegete na Oscar Joshua kuchukua
nafasi za Nizar na Bahanuzi kuliongeza uhai Yanga na matunda yake ni
kusawazisha bao dakika ya 82 kupitia kwa Kavumbangu, akimalizia krosi
David Luhende.
Kwa
matokeo hayo, Yanga inafikisha pointi tano baada ya kucheza mechi tatu,
ikitoa sare mbili na kushinda moja, sawa na Mbeya City ambao pia wana
pointi tano sasa baada ya sare mbili na kushinda mechi moja, zote
nyumbani.
Mapema
mashabiki wa Mbeya City walilitupia mawe basi la Yanga wakati linaingia
uwanjani na kusababisha kioo cha mbele upande wa dereva kuvunjika na
pia kumjeruhi dereva huyo.
Mwenyekiti
wa Yanga SC, Yussuf Manji alikuwa jukwaani kushuhudia mchezo huo pamoja
Makamu Mwenyekiti wake, Clement Sanga na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji,
Isaac Chanji na Mussa Katabro.
Kikosi
cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David
Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’,
Nizar Khalfan/Jerry Tegete dk59, Frank Domayo, Didier Kavumbangu,
Hussein Javu na Said Bahanuzi/Oscar Joshua dk59.
Mbeya
City; David Burhan, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Deogratius Julius,
Antony Matogolo, Yohana Morris, Mwagane Yeya, Steven Mazanda, Paul
Nonga/Fidelis Castor dk82, Deus Kaseke, Yussuf Willson/Alex Sethi dk 59.
Katika mechi nyingine za Ligi hiyo, Simba SC iliiendeleza wimbi la ushindi baada ya kuilaza Mtibwa Sugar 2-0.
Hadi
mapumziko, hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao na kipindi cha pili,
ndipo Wekundu wa Msimbazi walipong’ara, Henry Joseph akianza kufunga
dakika ya 70 na Betram Mombeki akafuatia dakika ya 90.
Simba
SC; Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’,
Kaze Gilbert, Joseph Owino, Jonas Mkude, Twaha Ibrahim/Betram Mombeki
dk64, Said Ndemla/Henry Joseph dk55, Amisi Tambwe, Amri Kiemba na Haroun
Chanongo/Ramadhan Singano dk77.
Mtibwa
Sugar; Hussein Sharrif ‘Casillas’, Hassan Ramadhani, Paul George,
Dickson Daudi, Salim Abdallah, Shaaban Nditi, Ally Shomary, Masoud
Mohamed/Awadh Juma dk58, Juma Luizio/Mussa Mgosi dk46, Shaaban
Kisiga/Abdallah Juma dk75na Vincent Barnabas.
Uwanja
wa Kaitaba mjini Bukoba, Themi Felix Buhaja alitangulia kuifungia
Kagera Sugar dakika ya 25 kabla ya Khamis Mcha ‘Vialli’ kuisawazishia
Azam FC dakika ya 55.
Katika
mechi nyingine Coastal Union ilitoka sare ya bila kufungana na Tanzania
Prisons Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Ruvu Shooting iliifunga 1-0 Mgambo
Shooting bao pekee la Elias Maguri dakika ya 53 Uwanja wa Mabatini
mkoani Pwani, Oljoro JKT ilitoka sare ya 1-1 Rhino Rangers Uwanja wa
Sheikh Amri Abeid, Arusha, wenyeji wakilazimika kusawazisha dakika ya 27
kupitia kwa Amiri Hamad baada ya Saad Kipanga kutangulia kuwafungia
wageni dakika ya tano, wakati Ashanti United ililala 1-0 mbele ya JKT
Ruvu, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam bao pekee la Amos Mgisa
dakika ya 81.
Matokeo
hayo, yanamaanisha JKT Ruvu inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi
zake tisa baada ya kushinda mechi zote tatu, ikifuatiwa na Simba SC
katika nafasi ya pili yenye pointi saba. Timu nyingi zimefungana kwa
pointi tano katika nafasi ya tatu, zikiwemo Yanga, Azam na Coastal
Union.
No comments:
Post a Comment