Kikosi cha Simba, kinachofundishwa na kocha Mkameruni Joseph Omog, kesho kitakuwa na kibarua kizoto wakati kitakapo wakabili mabingwa wa Kombe la Mapinduzi Azam FC, katika mchezo wa mzunguko wa 19 wa ligi ya Vodacom Tanzania Bara.
Huo ni mtihani mkubwa kwa kocha Omog na kikosi chake kwani endapo watapoteza au kutoka sare watakuwa wameiweka rehani nafasi ya kwanza walioishikilia kwa muda mrefu tangu kuanza kwa msimu huu.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0,  mfungaji akiwa Shizza Kichuya.
Azam ililipa kisasi kwa ushindi kama huo katika mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi uliopigwa uwanja wa Amani Zanzibar bao likifungwa dakika ya 13 na kiungo mkabaji Himid Mao.
Matokeo ya mechi hizo mbili yanaonyesha ugumu utakao kuwepo kwenye mchezo wa kesho ambao umepangwa kupigwa kwenye uwanja wa Taifa ambao utatumika kwa mara ya kwanza baada ya kufungiwa na Serikali kufuatia vurugu za mashabiki wa Simba Oktoba 1 mwaka 2017.
Simba ambayo mchezo uliopita ilitoka sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar, itahitaji ushindi ili kujiimarisha kileleni wakati Azam ambayo nayo ilipata sare ya bila kufungana na Mbeya City kesho itaendelea kuongozwa na Idd Cheche baada ya kocha wake mpya Akistica Cioaba kukosa kibali cha kufanyia kazi.
Simba imeiacha Azam kwa pointi 13, idadi ambayo ni kubwa na Azam wanalazimika kupambana kiume ili kuweza kupunguza pengo hilo na kushinda taji hilo kama walivyohitaji.
Mshambuliaji John Bocco, ambaye pia ndiye nahodha ameshajigamba kuwa ni lazima aifunge Simba katika mchezo huo kutokana na mbinu bora kutoka kwa kocha mpya Akistica Cioaba raia wa Romania.
Azam itakuwa ikimtegemea zaidi kipa wake Aishi Manula aliyemaliza michuano ya Kombe la Mapinduzi bila kuruhusu bao kwenye nyavu zake na kiungo wake Mcameroon Stephen Kingue ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wa kukaba.
Kocha wa Simba Omog, amepata faraja baada ya kiungo wake mshambuliaji Mohamed Ibrahim kupona majeraha ya kifundo cha mguu na kuanza mazoezi wiki hii.
Omog amesema anamatumaini makubwa na mchezaji huyo pamoja na mshambuliaji mpya Juma Luizio, ambao wamekuwa wakitoa presha kubwa kwa timu wanazokutana nazo.
Kocha Akistica Cioaba wa Azam amesema pamoja na kutokuwa sehemu ya mchezo huo lakini amewaelekeza kila kitu wachezaji wake na kocha Idd Cheche ikiwemo matumizi ya mfumo wa 4-3-3, ili kuwasoma wapinzani wake Simba na kufanya mashambulizi ya kustukiza kama ilivyokuwa kwa kocha aliyepita lakini kocha wa Somba amesema kwakuwa watacheza kwenye uwanja mkubwa kesho watafunguka kwa kucheza kwa kushambulia wakitumia mfumo wa 4-4-2, ili kupata ushindi.