tuwasiliane

Friday, January 27, 2017

Ligi ya Kenya kushirikisha timu 18 msimu ujao

Rais wa Shirikisho la soka nchini Kenya Nick Mwendwa
Ligi kuu ya soka nchini Kenya inatarajiwa kuwa na timu kumi na nane kutoka timu kumi na sita kuanzia msimu ujao baada ya kampuni inayosimamia ligi hiyo KPL na shirikisho la soka nchini Kenya FKF kuafikiana.
Pande hizo mbili zimekuwa zikitofautiana kwa muda kuhusu idadi ya timu zitakazoshiriki kwenye ligi tangu msimu uliopita na kusababisha kucheleweshwa kwa tarehe ya kuanzi kwa ligi.
Makubaliano hayo yaliafikiwa usiku wa kuamkia leo baada ya bodi ya kusikiliza malalamishi kwenye michezo, SDT, kuzipa pande hizo muda.
Hatua hiyo inaonekana kuwa ushindi kwa Rais wa shirikisho la soka nchini FKF, Nick Mwendwa ambaye amekuwa akitetea kuongezwa kwa idadi ya timu kwenye ligi hiyo.
Ingawa kampuni inayoendeesha ligi hiyo, KPL, imekuwa ikipinga hatua hiyo kutokana na kutokuwepo kwa pesa za kutosha, shirikisho hilo la soka limeahidi kutatua kikwazo hicho ili kufanikisha uamuzi wa kuwa na timu kumi nane kwenye ligi.
Awali shirikisho la soka liliziondoa timu tatu za Muhoroni Youth, Thika United, na Sofapaka kwa kutokamilisha usajili wao wa kutimiza masharti ya usajili na leseni za vilabu kulingana na FIFA na kusalia na timu 15.
Makubaliano hayo yamepatia matumaini timu hizo zilizopigwa upanga kuanzisha upya mikakati ya kusajiliwa tena ili kurejea kwenye ligi.
Maafisa wakuu watendaji wa KPL na FKF wanatarajiwa kuwa na vikao zaidi kuziba pengo la pesa na masuala mengine ya timu kwani shirikisho la FKF limeamua kutoka shilingi milioni 36 ili kuziwezesha timu mbili zaidi zilizoongezwa kushiriki kwenye ligi.

No comments:

Post a Comment