tuwasiliane

Friday, January 27, 2017

Shekhan Rashid: ‘Ulimwengu atafanikiwa Sweden kama ilivyokuwa kwa Michael Olunga…’

Miezi 18 iliyopita mshambulizi raia wa Kenya, MichaelOlunga aling’ara katika michuano ya Cecafa Kagame Cup 2015 jijini Dar es Salaam na baada ya Mkenya huyo aliyekuwa akichezea Gor Mahia kuibuka mfungaji bora wa michuano ile ya Julai, 2015 klabu kubwa nchini za Yanga SC na Simba SC zilishindana kuhakikisha zinamnasa Olunga lakini hazikufanikiwa kutokana na mchezaji mwenye na klabu yake wakati huo kuhitaji kiasi cha zaidi ya milioni 100 ili kucheza ligi kuu Tanzania Bara.
Baadae, Olunga alisajiliwa na klabuya Djurgardens ya Sweden ambayo kwa msimu mmoja alifanikiwa kufunga zaidi ya magoli kumi katika michezo 27 aliyochezea timu hiyo ya Sweden.
Olunga ameondoka Sweden na kujiunga na klabu ya Guizhou Zhicheng ya China kwa usajili wa rekodi katika soka la Sweden-Dola million 40 zaidi ya bilioni 80 za Kitanzania.
Olunga alicheza michezo michache sana hasa katika duru la pili kwenye ligi kuu ya Sweden msimu uliopita na kuifungia timu yake magoli muhimu.
Sasa anaenda China kuvuna pesa nyingi. Nakubaliana na wewe kuhusu ulichoandika (niliandika namna nilivyoshangazwa na usajili wa Thomas Ulimwengu kutoka TP Mazembe na kujiunga na klabu ya AFC ya Sweden ambayo imepanda daraja msimu huu na itacheza ligi kuu.)”
“Ni kweli Mazembe ni klabu kubwa ila napenda kukuambia Ulaya ni Ulaya tu, hata kama Mazembe wangekuwa wakimpa pesa nyingi, ila ujio wa Ulimwengu hapa Sweden nimzuri sana.
Ataonekana zaidi kuliko akibaki kucheza Afrika. Narudia tena kusema, hata kama AFC watakuwa wanamlipa pesa ndogo kuliko Mazembe lakini Ulaya ni Ulaya tu kama ukiwa na malengo,” nasema kiungo wa zamani wa Kimataifa wa Tanzania, Shekhan Rashid ambaye kwa sasa anaishi nchini Sweden.
Ulimwengu ameanza mazoezi katika klabu yake mpya AFC ambayo imesaini kwa mkataba wa miaka miwili kufuatia kushindwa kupata ofa alizotaraji kutoka klabu za Uturuki, Ubelgiji, na sehemu nyingine duniani.
Ikumbukwe Ulimwengu aliichezea AFC mwaka 2010 akiwa kama mchezaji wa timu ya vijana katika klabu hiyo ya Sweden.
“Nafasi kama hii siyo mbaya ikiwa amekosa ofa kutoka katika klabu za nchi nyingine kubwa kama Ufaransa ila kwa hapa Sweden akijituma kidogo tu atakwenda kwenye hizo nchi zenye ligi kubwa.
“Kikubwa ni kumpa sapoti ili afanikiwe katika malengo yake,” anasisitiza Shekhan mchezaji wa zamani wa Singida United, Simba SC, Mtibwa Sugar, Moro United na Azam FC.

No comments:

Post a Comment