tuwasiliane

Wednesday, December 7, 2016

Azam FC Academy yatinga nusu fainali Ligi ya Vijana

TIMU ya vijana ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetinga nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Taifa ya Vijana iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Azam FC U-20 ilitotinga nusu fainali baada ya kuitungua Mwadui mabao 5-0 Jumatano iliyopita, jana ilikamilisha ratiba kwa kuibanjua Toto African 4-0, yaliyofungwa kiufundi na nahodha wake, Abdallah Masoud aliyetupia mawili, Shaaban Idd na Salum Isihaka.
Timu hiyo iliyoonyesha ubora mkubwa mpaka sasa kwenye michuano hiyo, inatarajia kushuka dimbani Ijumaa ijayo kukipiga na Mtibwa Sugar katika mchezo wa nusu fainali utakaofanyika saa 1.00 usiku katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Mchezo huo utatanguliwa na mtanange mwingine wa nusu fainali ya kwanza, utakaozihusisha Simba na Stand United utkaopigwa saa 10.00 jioni ndani ya uwanja huo.
Hitimisho la michuano hiyo, iliyodhaminiwa na Kampuni ya Azam Media kupitia Azam TV, ambayo ilikuwa ikirusha moja kwa moja mechi, litafanyika Jumapili ijayo kwa mchezo wa fainali utakaopigwa saa 1.00 usiku ndani ya uwanja huo ukihusisha washindi wa nusu fainali hizo.
Kwa timu zitakazopoteza mechi zao za nusu fainali zitakutana katika mtanange wa kutafuta mshindi wa tatu, ambao nao utapigwa siku hiyo saa 10.00 jioni kabla ya mtanange wa fainali.
Azam FC U-20 inaingia kwenye raundi ya pili ya michuano hiyo, ikiwa imetoka kuongoza Kundi B lililokuwa kwenye kituo cha mjini Bukoba, mkoani Kagera ikimaliza na pointi 17 baada ya kushinda mechi tano na kutoa sare mbili pasipo kufungwa mchezo wowote.
Jambo la kufurahisha zaidi, ndiyo timu pekee kwenye michuano hiyo iliyofunga mabao mengi kuliko timu nyingine shiriki ikitupia kambani mara 17, ikiwa na wastani wa kufunga mabao mawili kila kila mchezo ndani ya mechi saba ilizocheza.
Mshambuliaji wake Shaaban Idd, aliyeng’ara kwenye michuano hiyo akiwa ni mmoja wa chezaji waliofunga ‘hat-trick’, ndiye anayeongoza kwa upachikaji mabao kwenye michuano hiyo mpaka sasa akiwa na amefunga saba, huku nahodha Abdallah Masoud akiwa nayo manne.

No comments:

Post a Comment