Mussa Hassani Mgosi
Timu Meneja wa klabu ya Simba Mussa Hassan ‘Mgosi ametoa ruhusa kwa kila mchezaji wa timu hiyo anayetaka kuondoka kuhamia timu nyingine ikiwemo Yanga aondoke kwasababu timu yao haina tabia ya kuwabania wachezaji.
Meneja huyo ameiambia Goal,  amekuwa akisikia maneno mengi mtaani kuhusu nyota wao wawili Ibrahim Ajibu na Nahodha wao Jonas Mkude, ambao wanatajwa kuwa mbioni kujiunga na Yanga baada ya kugoma kuongeza mkataba.
“Simba hatumzuii mchezaji yeyote kuondoka kwasababu hapa ni sawa na chuo wamepita wachezaji wengi wazuri nab ado hadi leo timu ipo na inafanya vizuri kwaiyo mchezaji anayeona Simba hapamfai anaweza kuondoka,”amesema Mgosi.

Kiongozi huyo amekiri kuwa Mkude na Ajibu ni wachezaji muhimu kwenye kikosi chao na wangependa kuwa nao siku zijazo lakini hawawezi kuwalazimisha kama wenyewe wameamua kwenda sehemu nyingine kutafuta kilicho kikubwa.
Mgosi amesema pamoja na kuyumba kwa misimu kadhaa, lakini timu yao imeanza kufufuka na kurudi kwenye ubora wake kama ilivyokuwa zamani kipindi ambacho wao walikuwa wanacheza na kuipa mafanikio timu hiyo.
“Unapotaja jina la Simba ni tofauti sana na timu nyingine ndogo ndogo unapoitaja Simba unazungumzia timu kubwa Afrika kama TP Mazembe, Al Ahly na Zamalek timu ambayo wachezaji wanaipigania ili kupata nafasi ya kusajiliwa,”amesema Mgosi.
Kiongozi huyo aliyewahi kucheza timu hiyo kwa mafanikio makubwa, amesema hawatambembeleza mchezaji kwakua kila mtu ndani ya kikosi chao anajitambua na anajua wajibu wake katika kufanikisha maendeleo ya timu .
Hata hivyo Mgosi amesema wachezaji hao ambao wanalalamikiwa wapo kikosini na wanaendelea na mazoezi ya kujandaa na mzunguko wa pili chini ya kocha wao Joseph Omog raia wa Cameroon.