tuwasiliane

Saturday, November 19, 2016

AFFUL;Subirini moto, tutakuwa tishio eneo la ushambuliaji’


NYOTA mpya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Samuel Afful, ameweka wazi kuwa kikosi hicho kitakuwa moto kuelekea michuano mbalimbali itakayoshiriki kuanzia mwezi ujao kutokana na ujio wake na aina ya wachezaji aliowaona ndani ya timu hiyo.
Mshambuliaji huyo kutoka Ghana amesaini mkataba wa miaka mitatu juzi akitokea timu ya Sekondi Hasaacas ya huko, anaungana na nyota wengine Waghana waliosajiliwa na Azam FC msimu huu, beki wa kati Daniel Amoah, winga Daniel Atta Agyei na mshambuliaji Yahaya Mohammed.
Afful, 20, alifunga bonge la bao kwa shuti kali kwenye mechi yake ya mwisho ya majaribio dhidi ya Ruvu Shooting Jumatatu iliyopita katika ushindi wa 3-1 wa Azam FC.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Afful alisema kwa aina ya wachezaji ambao Azam FC imewasajili kutoka Ghana akiwemo yeye basi itarajia kuwa na safu tishio ya ushambuliaji kwenye mechi zinazokuja.
“Nimefurahi sana kujiunga na Azam FC kama mchezaji mwingine anavyofurahia kusaini mkataba na timu mpya, namshukuru Mungu kwani yeye ndiye amefanikisha hili, nimejiandaa vilivyo kuisaidia timu hii na naamini kwa namna nilivyowaona wachezaji kwenye mechi mbili nilizocheza na usajili uliofanywa Azam FCitakuwa moto sana kwa mechi zinazokuja na eneo la ushambuliaji litakuwa tishio,” alisema.
Afful aliongeza kuwa: “Ni wapya kwenye timu lakini tutakapokuwa tukicheza wote tutakuwa tukizungumza lugha moja ya kusaidia timu kwenda mbele, naamini kwa aina ya wachezaji niliowaona na sisi tulioongezeka, Azam FC itakuwa na kikosi bora kabisa cha muhimu ni mashabiki kujitokeza kwa wingi kutusapoti, nilifurahishwa na ujio wao kwenye mechi ile iliyopita (Ruvu Shooting), hali hiyo inatupa nguvu sisi wachezaji.”
Alisema kuwa Azam FC imesajili watu sahihi kwa ajili ya kuimarisha kikosi huku akidai kuwa imebakia kwa upande wao kulipa fadhila kwa kufanya vema uwanjani.
Kinda huyo wa timu za Taifa za Ghana chini ya umri wa miaka 20 na 23, aliwahi kuchaguliwa kuwa mchezaji bora anayechipukia kutoka Ghana mwaka juzi, na anakuja Azam FC akiwa ametoka kufunga jumla ya mabao tisa kwenye Ligi Kuu ya Ghana msimu uliopita akiwa na Sekondi Hasaacas, Pia alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ghana anayechipukia mwaka juzi
Mbali na kuwepo timu hizo za vijana, atakumbukwa kwa rekodi aliyoweka mwaka jana ya kuifungia bao muhimu timu ya Taifa ya Ghana chini ya umri wa miaka 20 (U-20) ilipokuwa ikicheza na Zambia, kwenye ushindi wa mabao 2-1 na kuipa nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia nchini New Zealand, baada ya kutinga nusu fainali ya Mataifa ya Afrika kwa Vijana (U-20) zilizofanyika Senegal mwaka huo.
Afful pia amewahi kuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ghana cha wachezaji wa ndani, kilichoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zilizofanyika Ghana mwaka juzi na timu hiyo kushika nafasi ya pili akiwa sambamba na nyota mwingine aliyesajiliwa na Azam FC, Yahaya Mohamed.
Kikosi cha Azam FC kwa sasa kipo kwenye mapumziko ya wiki mbili hadi Desemba 3 mwaka huu, kitakapoanza mazoezi ya kwanza kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi pamoja na michuano mingine mbalimbali.

No comments:

Post a Comment