tuwasiliane

Saturday, November 19, 2016

Busungu azitaka Stand United na Mtibwa Sugar kufanya mazungumzo na Yanga

Malimi Busungu
Klabu za Stand United na Mtibwa Sugar zinapigana vikumbo kuwania saini ya mshambuliaji wa Yanga Malimi Busungu ambaye hivi karibuni alijiondoa kwenye timu hiyo kutokana na kuwekwa benchi.
Busungu amekiambia chanzo chetu kuwa, kwasasa hawezi kuzungumzia chochote kuhusiana na hilo kwasababu bado anamkataba na Yanga.
“Ninachojua mimi bado ni mchezaji halali wa Yanga kwahiyo siwezi kulizungumzia hilo na kama hizi timu zinanihitaji nivyema zikaenda kuzungumza na uongozi wangu,”amesema Busungu.
Mshambuliaji huyo ambaye hajaichezea Yanga kwa miezi minne, amesema amefurahi kuona timu hizo zikimuhitaji na hiyo ni wazi kwamba uwezo wake ni mkubwa na ndiyo maana zikajitokeza kumuhitaji.
Akizungumzia mipango yake ya baada ya kurejea kwenye kikosi cha Yanga amesema amejipanga kuonyesha uwezo mkubwa mazoezini ili kumshawishi kocha mpya George Lwandamina aweze kumpa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.
Amesema anaamini hilo linawezekana kwa sababu yeye ni mpambanaji mzuri na ndiyo maana Yanga walimsajili kutokana na juhudi zake alipokuwa Mgambo JKT ya Kabuku Tanga.
Busungu amesema anachukia kukaa benchi ndiyo maana aliondoka Yanga, lakini ujio wa kocha Lwandamina umemshawishi kurudi akiamini anaweza kumrudisha kwenye kikosi cha kwanza.
“Niliondoka kwasababu kocha Hans van der Pluijm, alishindwa kuniamini na kuniweka benchi kila mechi jambo ambalo halikunifurahisha kwasababu nimekuja Yanga kucheza siyo kukaa benchi,”amesema Busungu.
Busungu amesema atajitahidi kufanya kila liwezekanalo ili kuweza kubaki kwenye klabu hiyo ambayo anaipenda kutoka moyoni mwake.
Mshambuliaji huyo mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao amebakiza mezi sita ili kumaliza mkataba wake wa miaka miwili wa kuichezea Yanga.

No comments:

Post a Comment