Mshambuliaji wa Mwadui FC, Hassan Kabunda, yupo mbioni kujiunga na matajiri wa Azam FC, baada ya kocha wa timu hiyo Zebeni Hernandez kuvutiwa naye.
Katibu mkuu wa Mwadui Ramadhani Kilao, amekiambia chanzo kimoja, wameipokea ofa hiyo lakini hawapo tayari kumuachia chipukizi huyo kutokana na kuwa na mkataba wa muda mrefu na timu yao.
“Kweli tumepokea ofa kutoka kwa wenzetu Azam wakimtaka Kabunda, lakini hatupo tayari kumtoa mchezaji huyo kwasababu bado yupo kwenye mipango yetu na anamkataba wa muda mrefu wa kuichezea Mwadui,”amesema Kilao.
Kiongozi huyo amesema kwa kipindi hiki hawan mpango wa kuacha mchezaji hata mmoja kwenye kikosi chao kwasababu awali walisajili wachezaji 24 na kubakiwa na nafasi sita za kujaza.
Amesema kitu kingine kinachofanya kisimuuze mchezaji huyo ni mwenendo mbaya walioanza nao msimu huu, na Kabunda ndiyo mchezaji wao tegemezi kwenye safu ya ushambuliaji akishirikiana na mkongwe Jery Tegete.
“Tuna mapengo mengi ya kujaza ndiyo maana tumepanga tusiache mchezaji yeyote kwenye kipindi hiki cha usajili mdogo ispokuwa tumepanga kuongeza wachezaji wengine ili kujenga kikosi cha ushindani,” amesema Kilao.
Kiongozi huyo amesema tayari kuna wachezaji wengi ambao wamezungumza nao kwa ajili ya kuwasajili na sasa wapo kwenye kukamilisha taratibu za usajili wao kabla ya dirisha kufunga.
Kiongozi huyo amesema mikakati yao ni kurudi kwa kasi mzunguko wa pili na kurudi kwenye ubora wao waliokuwa nao kwenye msimu wakwanza ambao walifanya vizuri na kuzisumbua baadhi ya timu kubwa.
Kabunda ndiyo mfungaji wa bao pekee, la Mwadui ilipocheza na Azam FC, kwenye mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza ambao wageni walipata ushindi wa mabao 4-1.
No comments:
Post a Comment