KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeendelea kujiongezea umaarufu na kutengeneza jina lake Kimataifa kila kukicha kadiri miaka inavyosogea.
Baada ya kuanza kwa kushika namba moja kwa ubora nchini Tanzania kwa mujibu wa mtandao wawww.footballdatabase.com ikiwa nafasi ya 337 miongoni mwa timu za Afrika ikifuatiwa na Simba kwenye nafasi ya 342.
Safari hii inaelekea kunufaika na ziara yake ya kushiriki michuano maalumu inayoendelea jijini Ndola nchini Zambia baada ya kuzivutia klabu za Zesco United na Zanaco (Zambia) pamoja na mabingwa wa Zimbabwe, Chicken Inn, ambao wameonyesha dhamira yao ya kuja Tanzania.
Akizungumza na mtandao wa klabu hiyo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema timu zote tatu zimeonyesha nia ya kuja Tanzania kucheza nasi pamoja na kujifunza namna tunavyoendesha timu yetu.
“Tunawashukuru waandaaji wa michuano hiyo kwa kutupa nafasi na tumeona kuwa klabu yetu ina heshima, sasa hivi watu wanaiheshimu na wanaona kabisa kuna kitu tofauti cha kujifunza kutoka Azam FC tofauti na huko nyuma na vilabu vingine, tofauti na mpira ulivyokuwa ukiendeshwa huko nyuma na klabu nyingine,” alisema.
“Na vilabu vyote hivi vinavyoshiriki michuano hii kwa ufasaha kabisa vimeonyesha dhamira ya kuja Dar es Salaam, kuja kucheza na sisi na kuja kujifunza sisi tunafanya nini, tunaendeshaje mpira na tuna kitu gani Azam FC, kile ambacho tunaona ni tofauti kwao na tumewapa nafasi hiyo ya kuja Dar es Salaam, kwa hiyo tutegemee klabu kama Zesco itakapokuwa inakwenda kucheza Sudan Kusini kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika (AL Ghazala Wau FC) wanaweza kuweka kambi Dar es Salaam, tutegemee Chicken Inn kuja Dar es Salaam, tunategemea Zanaco nayo kuja Dar es Salaam,” alisema.
Kawemba alifungua milango kwa klabu nyingine yoyote ambayo inapenda kujifunza kupitia Azam FC na kuongeza kuwa: “Kwa hiyo ni faraja kwetu kuona kwamba kuna vilabu kutoka nje ya nchi vinataka kujifunza kutoka Azam FC na hatushangai kuona watu nyumbani hawawezi kujifunza kutoka kwetu, lakini muda utafika na watu wa nyumbani wataona kuna kitu tofauti Azam FC na watakuja kujifunza.”
Azam FC mpaka sasa ipo kileleni kwenye michuano hiyo kwa pointi nne sawa na Zanaco, hii ni baada ya kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Zesco United katika mchezo wa ufunguzi kabla ya kuichapa Chicken Inn mabao 3-1.
Hali ya timu Zambia
Akizungumzia hali ya kikosi hicho wakiwa nchini humo, Kawemba alisema wanaendelea vema na ziara yao na kueleza kuwa wamekutana na uwanja (Levy Mwanawasa) wanaoutumia kwa michuano hiyo, unaofanana kabisa na ule wanaoutumia Bidvest Wits ya Afrika Kusini, timu ambayo wana nafasi kubwa ya kukutana nayo katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika mwezi ujao.
“Kwanza tunamshukuru Mwenyezi Mungu, ziara yetu inaendelea vizuri na uwajibikaji wa timu umekuwa ni mzuri, hali ya hewa ina changamoto (baridi), lakini kwa maana ya mazoezi pia ni nzuri, hali ya uwanja ni nzuri, tunasema kabisa ya kwamba tumeukuta uwanja ambao nyasi zake na mazingira yake ya uwanja, yanafanana moja kwa moja na uwanja ambao tutauchezea endapo kama Bidvest Wits itavuka, hivyo tunajivunia kupata bahati hiyo,” alisema.
Mchezo wa mwisho vs Zanaco
Kawemba alisema mchezo wao wa mwisho wa michuano hiyo dhidi ya Zanaco FC utakaofanyika kesho saa 10.00 jioni unatarajia kuwa mgumu kwa sababu utakuwa ni mchezo wa fainali, ambao utatoa bingwa wa mashindano hayo.
“Hii ni kama ulivyokuwa mchezo wa mwisho msimu uliopita kwenye michuano hii wakati tukiwa Lubumbashi (DR Congo) kati ya Zesco United na TP Mazembe, ilikuwa ni mechi ya kuamua bingwa, kwa hiyo mechi yetu hiyo dhidi ya Zanaco ndio itakayotoa nani atakuwa ni mshindi na sisi tunahitaji sare kwa sababu itatupa faida ya kuwa na tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa, lakini pia tunahitaji kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri zaidi, hii itatusaidia zaidi kuona kwamba tunafanya namna tumaposhiriki michuano ya Kimataifa na namna gani ya kucheza kila tunapokutana na timu za aina hii.
“Tunashukuru sana viongozi wetu kwa kuweza kufanikisha hili, tunawashukuru viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa sababu walituelewa na kuweza kuturuhusu sisi kuja huku na washabiki wetu wote wa Azam FC popote pale walipo tunawaambia kwamba waendelee kuwa watulivu, timu ipo salama na itakaporejea nyumbani baada ya mashindano haya, tutaendelea na hatua ile ile pale tulipoishia ndio utakuwa ni utaratibu wetu kuhakikisha kwamba pointi tatu muhimu katika kila mchezo inakuwa ndio haswa lengo letu,” alisema.
Awatoa hofu mashabiki
Kawemba aliwatoa hofu mashabiki wa Azam FC kuhusiana na mechi zao za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) watakazocheza baada ya kurejea Dar es Salaam kwa kusema kuwa hawatakuwa na matatizo yoyote kuelekea mechi zao nne watakazocheza dhidi ya Mwadui FC Jumapili hii, Coastal Union (Tanga) na mechi mbili nyingine watakazokipiga jijini Mbeya na Mbeya City na Tanzania Prisons.
“Ni pointi 12 katika mechi nne, ni kitu kinachowezekana hiyo ni dhamira yetu na hatuna rekodi mbaya tunapocheza ugenini, hivyo tunaamini ya kwamba mazoezi haya tunayofanya huku kwa sababu ni ya juu zaidi ya ligi tnayokwenda kuicheza haitatupa tabu yoyote, kwa hiyo hatuna tatizo na hilo hata kidogo,” alisema.
No comments:
Post a Comment