Mwanafunzi Mtanzania alishambuliwa na kuvuliwa nguo na umati uliokuwa na hamaki katika jiji la Bangalore, kusini mwa India.
Alishambuliwa baada ya gari la mwanafunzi kutoka Sudan kumgonga na kumuua mwanamke mmoja eneo hilo.
Umati ulimvamia mwanafunzi huyo wa kike wa umri wa miaka 21 pamoja na marafiki wenzake watatu, wote kutoka Tanzania.
Walikuwa wakipitia eneo hilo muda mfupi baada ya ajali kutokea.
Umati ulimkimbiza mwanamke huyo na “kumvua blauzi”, polisi wamesema.
Ubalozi wa Tanzania umeitisha taarifa kuhusu kisa hicho, ripoti zinasema.
Kisa hicho kilitokea usiku wa Jumapili, lakini kiliripotiwa mara ya kwanza Jumanne.
Polisi wameambia mwandishi wa BBC Hindi, Imran Qureshi mjini Bangalore kwamba umati ulikusanyika eneo la Hessarghatta baada ya mwanafunzi kutoka Sudan aliyekuwa amelewa kumkanyaga mwanamke aliyekuwa amelala pembeni mwa barabara akiwa na gari lake.
Mwanafunzi huyo kutoka Sudan alipigwa na gari lake kuteketezwa lakini alifanikiwa kutoroka.
"Dakika 30 baadaye, wanafunzi wanne (kutoka Tanzania), walikuwa wakipita waliposimama na kuuliza kilichotokea. Ndipo waliposhambuliwa,” Bernandoo Kafumu, rais wa chama cha wanafunzi wa Tanzania katika chuo kimoja huko amesema.
“Mwanamke huyo hata hakumfahamu mwanamume huyo (wa Sudan) aliyehusika katika ajali hiyo,” mwanachama wa chama hicho cha wanafunzi ambaye hakutaka kutajwa amesema.
"Baada yao kushambuliwa, Watanzania hao walikimbia hadi kwenye gari lao na kujaribu kutoroka. Lakini kulikuwa na kizuizi, na walishuka na kukimbia kwa miguu. Alikimbilia maisha yake. Wenyeji walimkimbiza na kumvua nguo,” ameongeza.
Watu hao pia waliteketeza gari hilo.
Afisa wa ngazi ya juu wa polisi amethibitisha kwamba "blauzi yake iliraruliwa na kuvuliwa, lakini hakunyanyaswa kingono”.
"Baada ya habari kutokea kwenye vyombo vya habari Jumatano, tulimuomba (mwanafunzi huyo) kuwasilisha rasmi malalamishi. Tunafuata taratibu zote, atachunguzwa na daktari,” TR Suresh, naibu kamishna wa polisi wa Bangalore kaskazini, ameambia BBC Hindi.
Bangalore, ina mamia ya wanafunzi wa kigeni, wakiwemo 150 kutoka Tanzania.
No comments:
Post a Comment