tuwasiliane

Wednesday, January 6, 2016

AZAM VS YANGA HAKUNA MBABE

Wachezaji wa Azam FC na Yanga SC katika 'timbwili' wakati wa mchezo wao wa Mapinduzi Cup
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC imelazimishwa sare nyingine ya bao 1-1 dhidi ya Yanga usiku wa kuamkia leo kwenye mchezo wa pili wa michuano ya Kombe la Mapinduzi uliofanyika Uwanja wa Amaan Zanzibar.
Hiyo ni sare ya pili kwa Azam FC ndani ya michuano hiyo, ya kwanza ikiipata dhidi ya Mtibwa Sugar (1-1) katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi B.
Hivyo Azam FC inatakiwa kupata ushindi mnono kwenye mchezo wa mwisho wa makundi watakapocheza na Mafunzo ili kujihakikishia kusonga mbele kwa hatua ya nusu fainali.
Kocha wa Azam FC, Stewart Hall, alikifanyia mabadiliko saba kikosi chake tofauti na kile kilichocheza mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar, akiwaanzisha kipa Aishi Manula, mabeki Pascal Wawa, Shomari Kapombe, Racine Diouf, Jean Mugiraneza ‘Migi’, John Bocco, Kipre Tchetche.
Wachezaji pekee aliowabakisha kwenye kikosi hicho kilichoanza na beki Abdallah Kheri ‘Sebo’, kiungo Himid Mao ‘Ninja’, mshambuliaji Ame Ally ‘Zungu’ na winga Ramadhan Singano ‘Messi’.Azam FC ilianza vema mchezo huo, ambapo ingeweza kupata bao la kwanza dakika 18 baada ya winga Ramadhan Singano ‘Messi’ kupenyezewa pasi safi ya Kipre Tchetche, lakini shuti alilopiga wakati akitazamana na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ lilipaa pembeni ya lango.
Dakika ya 32 Tchetche naye alikosa bao jingine la kuipa uongozi Azam FC baada ya kupiga shuti lililopaa juu ya lango la Yanga, Tchetche alipata nafasi hiyo baada ya kupewa pasi nzuri na beki Shomari Kapombe, aliyewahadaa wachezaji kadhaa wa Yanga.Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, timu zote mbili zilienda vyumbani milango ikiwa migumu. Kipindi cha pili Azam FC ilianza kwa kufanya mabadiliko kwa kutoka Ame Ally na kuinia Mudathir Yahya.
Mabadiliko hayo yalizidi kuiimarisha Azam FC kwenye eneo la kiungo kwa Mudathir kuwaongezea nguvu Himid Mao na Jean Mugiraneza, ambao waliweza kuwadhibiti vilivyo viungo wa Yanga, Thabani Kamusoko na Mbuyu Twite.
Dakika ya 58 Azam FC iliandika bao la kwanza kupitia Tchetche aliyepokea pande safi la Mudathir na kuwakimbiza mabeki wa Yanga kabla ya kupiga shuti la ufundi mbele ya wachezaji watatu wa Yanga lililomshinda kipa.
Dakika ya 62 mwamuzi wa mchezo wa leo, Mfaume Ally, alifanya uamuzi wa kumtoa kwa kadi nyekundu nahodha wa Azam FC, John Bocco, aliyetemewa mate kwa makusudi na beki wa Yanga, Kelvin Yondani. Mwamuzi alichukua uamuzi huo baada ya kuitwa na mwamuzi msaidizi namba moja na kupewa maelekezo.
Cha kushangaza zaidi mwamuzi huyo alishindwa kumpa kadi nyekundu mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma, aliyempiga kwa makusudi na kumkanyaga nahodha msaidizi wa Azam FC, Himid Mao.
Azam FC ililazimika kucheza pungufu kwa takribani dakika 33, 28 za kumalizia dakika 90 na dakika tano zilizoongezwa, lakini iliweza kwa kiasi kikubwa kuibana Yanga, ambayo ilipata bao lenye utata dakika ya 83 lililofungwa na Vincent Bossou.
Hadi dakika 90 zinamalizika, timu hizo zilitoshana nguvu kwa sare hiyo ya bao 1-1, ambapo Azam FC imefikisha pointi mbili huku Yanga na Mtibwa Sugar zikiwa zimejikusanyia jumla ya pointi nne kila mmoja, Mafunzo ndio pekee ambayo haijaambulia pointi yoyote mpaka sasa ikiwa imefungwa mechi zote mbili.
Mechi za mwisho za Kundi B zitakazofanyika kesho Alhamisi zinatarajia kuamua hatima za timu zitakazofuzu kwa nusu fainali, ambapo Azam FC inayohitaji ushindi ili kusonga mbele itacheza na Mafunzo huku Yanga ikichuana na Mtibwa Sugar.

No comments:

Post a Comment