tuwasiliane

Wednesday, December 9, 2015

Stand United: "Elias Maguri hauzwi"

Elias Maguri
Baada ya Maguri kuonyesha uwezo wake kwa kupachika dazeni za mabao Ligi Kuu na kwenye timu ya taifa timu kadhaa zimekuwa zikimtolea macho.
Yanga na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo zimekuwa zikitajwa kutaka kumsajili nyota huyo wa Stand United.
Uongozi wa Stand United, umetangaza kuwa, klabu yoyote inayofanya mchakato wa kumsajili straika wao, Elias Maguri kwa sasa inajisumbua kutokana na kwamba bado wanamuhitaji huku mkataba wake ukitajwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Timu ambazo zimekuwa zikihusishwa na kuihitaji saini ya Maguri ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga na mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe ya DR Congo ambayo kesho Alhamisi itaanza harakati zake za kuwania Kombe la Dunia la Klabu huko Japan.
Ofisa Habari wa Stand United, Deokaji Makomba, amesema wamekuwa wakisikia taarifa za kutakiwa straika wao huyo lakini hakuna hata timu moja iliyowafuata kuzungumza nao, lakini akatoa angalizo kuwa hawapo tayari kumuachia kwa sasa kwani wanaihitaji huduma yake.
“Maguri bado ni mchezaji wetu na ataendelea kuwa wetu mpaka pale mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu.

“Tumesikia tetesi nyingi zikimhusu Maguri kutakiwa na timu nyingi tu, lakini kati ya hizo hakuna hata moja iliyokuja kuzungumza nasi kuhusiana na mchezaji huyo, lakini ieleweke tu hatupo tayari kumuachia kwa sasa na hata kama mkataba wake ukimalizika na tukiona bado tunamhitaji, tutakaa naye chini kujadili masuala ya mkataba mpya,” alisema Makomba akihojiwa na Saleh Jembe.

No comments:

Post a Comment