Ivo Mapunda, Kipa wa Azam FC
Kipa wa Azam FC, Ivo Mapunda ameeleza kuwa bado ana kiu ya kucheza soka la kulipwa.
Kipa mpya mkongwe wa Azam FC, Ivo Mapunda, amepanga kutumia michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (Caf) kwa ajili ya kujitangaza kimataifa ili apate nafasi ya kucheza soka la kulipwa.
Mkongwe huyo, alijiunga na Azam FC kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu wa Ligi Kuu Bara akitokea Simba inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.
Ujio wake kipa huyo kwenye kikosi cha Muingereza, Stewart Hall, utaongeza ushindani kwa makipa wa timu hiyo aliowakuta ambao ni Aishi Manula na Mwadini Ally.
Ivo amesema kuwa ana misimu miwili hajacheza michuano ya kimataifa akiwa Simba, hivyo amepanga kuitumia kwa ajili kujitengenezea soka kwenye klabu za nje ya nchi.
Ivo alisema, michuano hiyo inashirikisha klabu kubwa hivyo anaamini kama akiitumia vizuri, basi kuna uwezekano wa kupata dili la kwenda kucheza nje ya nchi kutokana na uwezo wake mkubwa alionao wa kuokoa michomo golini.
Aliongeza kuwa, katika hilo, anaamini atafanikiwa kutokana na safu bora ya ulinzi iliyopo Azam ikiongozwa na Muivory Coast, Pascal Wawa na Aggrey Morris.
“Azam nataka kuitumia kama njia ya kujitengezea soko la kucheza soka la kimataifa kutokana na ushiriki wa michuano ya kimataifa tutakayoshiriki, mwakani.
“Ninajua haitakuwa rahisi kwangu kujitengenezea soko la kucheza soka la kimataifa bila ya bidii na kujituma kwangu ndani ya uwanja, hivyo napanga kuitumia michuano hiyo kujitangaza,” alisema Ivo.