tuwasiliane

Tuesday, December 29, 2015

Hall aitangazia vita Mtibwa Sugar, aielezea michuano Mapinduzi Cup

KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa ushindi ni lazima katika mchezo wa kesho dhidi ya Mtibwa Sugar, ili kurejea kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 32, itamenyana na timu hiyo katika mchezo wake wa kiporo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, ushindi wowote utawafanya kufikisha pointi 35 na kuiteremsha Yanga iliyojikusanyia 33 kileleni.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, Hall alisema mipango yao ni kushinda mchezo huo huku akikiri kuwa utakuwa mgumu, lakini amedai wamejipanga kukabiliana na changamoto zote kutoka kwa wapinzani wao.
“Tumejipanga kushinda na lazima tufanye hivyo, tunataka kurejea namba moja kwenye msimamo, najua mchezo utakuwa mgumu kama ulivyokuwa kwa Kagera Sugar, lakini tumejipanga kwa changamoto zozote uwanjani,” alisema.
Hall aliongeza kuwa atawakosa wachezaji watatu walio majeruhi, ambao ni mabeki Aggrey Morris na Erasto Nyoni aliyeumia nyama za juu ya paja katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar, mshambuliaji Ame Ally ‘Zungu’, huku pia beki David Mwantika naye akikosekana baada ya kufiwa na mdogo wake mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mara ya mwisho Azam FC kucheza na Mtibwa Sugar kwenye uwanja huo, ilikuwa ni Februari mwaka huu walipoichapa mabao 5-2 na ziliporudiana Uwanja wa Manungu, zilitoka sare ya bao 1-1.
Programu ya Mapinduzi Cup
Katika hatua nyingine, Hall amefurahishwa na ratiba ya Kombe la Mapinduzi iliyopangwa jana, huku akisema kuwa ataitumia michuano hiyo kuwapa kipaumbele cha kucheza wachezaji ambao hawajacheza msimu huu.
Azam FC imepangwa Kundi B kwenye michuano hiyo sambamba na timu nyingine za Yanga, Mtibwa Sugar ya Morogoro na Mafunzo ya Zanzibar,
Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, watafungua dimba kwa kucheza na Mtibwa Sugar saa 2.15 usiku Jumapili hii, itacheza na Yanga Jumanne ijayo saa 2.15 usiku kabla ya kumaliza mchezo wa mwisho wa makundi kwa kuchuana na Mafunzo Januari 7, mwakani.
Vinara wawili wa kundi hilo na la lile la A lenye timu za Simba, Jamhuri, JKU na URA, watafuzu kwa hatua ya nusu fainali itakayochezwa kwa siku mbili Januari 9 na 10 (zote saa 2.15 usiku), huku mchezo wa fainali  ukipigwa Januari 13, mwakani.
“Ratiba iko vizuri, tunatakiwa kucheza na Mtibwa Sugar, Yanga na Mafunzo, kwetu sisi tutaitumia michuano ya Mapinduzi kuwapa kipaumbele cha kucheza wachezaji ambao hawajacheza mpira msimu huu, nataka kuona wakicheza Ame Ally, Allan Wanga, Messi (Ramadhan Singano), Gardiel Michael, Vialli (Khamis Mcha), Mudathir (Yahya), pia David Mwantika naye atakuwa amerejea.
“Nataka kuona wachezaji hao wakicheza, ni wachezaji wazuri na tunatakiwa kuwaweka fiti na kuwahamasisha kupitia Kombe la Mapinduzi,” alisema.
Msimu huu, Azam FC imepania kubeba vikombe kwenye michuano yote inayoshiriki kuanzia Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kombe la FA na Mapinduzi Cup, huku ikipanga kujiwekea rekodi ya kufika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Mara ya mwisho Azam FC kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi ilikuwa ni mwaka 2013, walipowafunga wageni waalikwa Tusker ya Kenya mabao 2-1 katika fainali, mabao yaliyofungwa na wachezaji wa zamani wa timu hiyo, beki raia wa Kenya Joackins Atudo na mshambuliaji Gaudence Mwaikimba.

No comments:

Post a Comment