tuwasiliane

Monday, June 23, 2014

SIMBA SC YAMSAJILI CHABALALA WA KAGERA SUGAR MIAKA MITATU

KAZI inaendelea. Simba SC imesajili mchezaji wa pili kwa ajili ya msimu ujao, ambaye ni chipukizi wa Kagera Sugar ya Bukoba, Mohammed Hussein Mohammed ‘Chabalala’. Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 19, anacheza beki ya kushoto na miongoni mwa wachezaji waliong’ara katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita akiwa na Wakata Miwa hao wa Misenyi. Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amekiambia Chanzo chetu leo kwamba, Chabalala amesaini Mkataba wa miaka mitatu.

 Kama nilivyosema, tuna muda mfupi sana kwa ajili ya kufanya usajili, tunafanyia kazi orodha ya wachezaji waliopendekezwa kwa kumalizana nao, ndani na nje ya nchi. Baada ya Joram (Mgeveke), sasa ni Chabalala,”alisema Poppe.   

Poppe amewahakikishia wana Simba SC kwamba safari hii watasajili wachezaji bora ambao watarejesha heshima ya klabu hiyo msimu ujao. Jana Simba SC ilikamilisha usajili wa beki wa kati, Joram Mgeveke wa Lipuli ya Iringa ambaye yupo katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Beki huyo alicheza kwa dakika 75 mechi ya kirafiki ya Tanzania na Malawi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambayo bao pekee la Amri Kiemba wa Simba SC liliipa Taifa Stars ushindi wa 1-0 kabla ya kumpisha Kevin Yondan wa Yanga. Tangu hapo, kinda huyo wa miaka 22 amekuwemo kwenye orodha ya wachezaji 18 walioshiriki mechi zote za Stars dhidi ya Zimbabwe kufuzu Mataifa ya Afrika kama mchezaji wa akiba.

No comments:

Post a Comment