MMOJA wa wagombea wa nafasi ya Urais kwenye uchaguzi ujao wa Simba, amepanga kumrejesha nchini kocha wa zamani wa timu hiyo, Milovan Cirkovic endapo akishinda kiti hicho.
Simba inajiandaa kwa uchaguzi mkuu uliopangwa
kufanyika Juni 29 jijini Dar es Salaam ambapo leo Jumamosi kamati ya
uchaguzi itakutana kuhakiki fomu za wagombea Jumatatu majina halisi
yatatangazwa kabla ya kuanza kupokea pingamizi Jumatano.
Habari za ndani kutoka kwenye kambi ya mgombea
huyo maarufu na mwenye wapambe wengi wanaojipa nafasi kubwa ya kushinda,
zinasema kwamba wao wana imani kubwa na Milovan zaidi ya kocha wa sasa,
Zdravko Logarusic.
Ingawa mgombea huyo alipobanwa na Mwanaspoti
aligoma kunukuliwa kwa kuhofia kukatwa jina lake kwavile kampeni
hazijaanza, Milovan alisema yupo tayari kurejea nchini kuifundisha Simba
ingawa hakuna kiongozi yoyote aliyempigia simuhadi sasa.
Cirkovic aliyewahi kuinoa Simba kabla ya ujio wa
Patrick Liewig msimu wa 2012/13, kwa sasa anaifundisha timu ya Taifa ya
Myanmar ambayo iko kambini Thailand kujiandaa na mechi ya Kombe la
Chalenji la Asia dhidi ya Maldives.
Kocha huyo alisema; “Nipo tayari kuachana na
Myanmar ili nije kuifundisha Simba kama viongozi watakubaliana na mimi
kuhusu maslahi na wakiniboreshea mkataba.”
Kabla ya kuondoka nchini, Logarusic ambaye mkataba
wake wa miezi sita unafikia tamati mwishoni mwa mwezi huu, alifikia
makubaliano ya kuendelea kuifundisha Simba na uongozi lakini kwa sharti
la kusaini mkataba Julai atakaporejea.
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga ameliambia
Mwanaspoti ; “Kweli tulikubaliana baadhi ya vitu na Logarusic, lakini
uongozi mpya ndiyo utakaoamua kama utaendelea naye au vinginevyo maana
wao ndiyo wakaomlipa.”
source.www.mwanaspoti.co.tz
source.www.mwanaspoti.co.tz
No comments:
Post a Comment