KIKOSI cha Yanga kimeanza kujifua jana Ijumaa katika kambi yake nchini Uturuki na leo Jumamosi mchana kitacheza mechi ya kirafiki na klabu ya Ankara Sekerspor inayoshiriki Ligi Daraja la Pili, Uturuki.
Yanga ikiwa chini ya Kocha Msaidizi, Boniface
Mkwasa ipo Uturuki kwa kambi ya wiki mbili kujiandaa na mzunguko wa pili
wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Msafara wa watu 33 wa Yanga unaojumuisha wachezaji
27 na viongozi sita, umefikia katika Hoteli ya Sueno Beach Side iliyopo
katika mji wa Antalya na jana Ijumaa mchana Mkwasa alianza kuinoa timu
hiyo kwenye uwanja wenye nyasi za kisasa ambao hata wachezaji
walionekana kufurahia na kutamani ungekuwepo Tanzania.
Baada ya mazoezi hayo, leo Jumamosi saa 8:00
mchana kwa saa za Afrika Mashariki, Yanga itacheza mechi ya kirafiki
dhidi ya timu ya Ankara Seker Spor katika kitongoji cha Manavgat lengo
likiwa ni kujiweka sawa.
Wachezaji wa Yanga wameonekana kuzoea hali ya hewa
mapema ingawa kuna kibaridi cha aina yake. Kwa hali ilivyo sasa mjini
Antalya mchana ni nyuzi joto 18c na usiku ni nyuzi joto 6c. Kwa kipindi
kirefu sasa jijini Dar es Salaam hali ya hewa wakati wa mchana ni nyuzi
joto 36c na usiku 29c.
Akizungumza na CHANZO CHETU, Ofisa Habari wa Yanga,
Baraka Kizuguto, alisema wachezaji wote wapo sawa na hakuna majeruhi
hata mmoja hivyo Mkwasa ana jukumu la kuwaweka fiti vijana wake.
“Tunacheza mechi ya kirafiki ili kujiweka sawa, hakuna mchezaji aliyelalamika kuhusu hali ya hewa,” alisema Kizuguto.
Mkwasa anaiongoza Yanga baada ya Ernest Brandts
kusitishiwa mkataba sambamba na msaidizi wake Felix Minziro na kocha wa
makipa Razack Siwa. Juma Pondamali ndiye aliyechukua nafasi ya Siwa.
Yanga inatazamia kutangaza kocha mpya muda wowote.
No comments:
Post a Comment