WAKALA wa Shomari Kapombe, Dennis Kadito amesema mchezaji huyo anaweza kupata uhalali wa kucheza timu yoyote ya Tanzania, lakini anatakiwa asubiri uamuzi wa kesi iliyofunguliwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Kapombe amegoma kurudi Ufaransa kwenye timu yake ya AS Cannes.
Rafiki wa karibu wa beki huyo ambaye ni kiongozi
mkubwa wa Simba ameiambia Mwanaspoti kuwa Kapombe kafikia uamuzi huo
baada ya AS Cannes kushindwa kumlipa mshahara na kwa muda sasa wamekuwa
wakimlipa nusu mshahara kiasi ambacho hakimtoshi kwa matumizi.
Kwa upande wake, Kadito amesema wamefungua kesi
Fifa wakipinga uamuzi wa Cannes kushinikiza Shirikisho la Soka la
Tanzania (TFF) limlipe Kapombe mshahara kwa muda wote aliokuwa nchini.
Lakini, Mwanaspoti linajua kuwa hata vibali vya
kuishi nchini humo vimekuwa tatizo kwa Kapombe kitu ambacho kimemfanya
ajisikie kama asiyethaminiwa.
Habari za ndani zinadai sababu nyingine ya Kapombe
kugoma ni baada ya klabu yake kuamua kuwa TFF ndio watakaomlipa
mshahara kwa kipindi chote alichobaki hapa nchini baada ya kuja
kuichezea Taifa Stars dhidi ya Zimbabwe mwishoni mwa mwaka jana, katika
mchezo wa kirafiki ambao Stars ililala kwa bao 1-0.
Wakala Kadito
“Ni kweli kuna matatizo hayo, kwa muda mrefu
Kapombe amekuwa akilipwa nusu mshahara, alivyofika huku alikuwa hana
akaunti, uongozi wa timu ulisema hautaweza kumlipa fedha zote
anazotakiwa kulipwa bila ya kuwa na akaunti ambayo pia isingeweza
kupatikana mpaka angepata viza ya kudumu ambayo ilikuwa ikihangaikiwa.
“Ilichukua muda mpaka kupatikana kwake na aliipata
Novemba mwaka jana, mwezi huo alilipwa mshahara mzima lakini fedha
alizokuwa akilipwa nusu ndiyo Cannes walikuwa wakishughulikia kuona
wanamlipa na wakati huohuo ndio alikuja huko Tanzania,” alisema Kadito
ambaye yupo Uholanzi.
Matatizo ya TFF
“Kulikuwa na matatizo yaliyosababishwa na TFF
iliyopita, kwanza walimpatia tiketi ya ndege yenye matatizo, kutoka
Tanzania mpaka Paris, Ufaransa kitu ambacho hakikuwa sahihi wakati
kulikuwa na uwezekano wa kumtafutia ile ya moja kwa moja mpaka Cannes
yalipo makazi ya timu. Niliwaambia kama watamleta Kapombe Tanzania kwa
viza ambayo alikuwa akiitumia awali anaweza kupata shida wakati wa
kurudi.
“Lakini wao wakafanya mipango yao bila
kunishirikisha, matokeo yake nilichowaambia awali ndicho kilichotokea,
Kapombe alifika mpaka Nairobi, Kenya akianza safari ya kurudi Ufaransa
lakini akakwama kutokana na matatizo hayo.
“Awali kocha Kim Poulsen alinieleza juu ya kumhitaji Kapombe,
nikamwambia kwa kipindi kile hakuwa sawa sana, wamuache kwanza lakini
hakuniamini akaona kama nafanya njama ya kumzuia nikishirikiana na
Cannes, ilinibidi nimtumie picha ya kidole ambacho alikuwa akikiuguza
ili ajiridhishe,”alisema Kadito.
“Nilimshauri Kapombe baada ya kuniambia hataweza
kurudi tena Ufaransa mpaka ajue hatma ya fedha zake, nikamwambia kwamba
ingekuwa busara angerudi kule kuendelea na timu wakati ambao wao
wanahangaikia malipo yake, unajua Cannes hawajakataa kumlipa
wanachokasirika wao ni kutokuwepo katika timu kwa Kapombe.
“Leo (jana Ijumaa) nimezungumza na AS Cannes
wanalalamika wametumia gharama kubwa kumtibu Kapombe, lakini ameanza
kupona bila ya kuitumikia klabu kitu ambacho kimewakera na sasa
wanaangalia uwezekano wa kuvunja mkataba au kumuuza, wamesema hawana
tatizo katika kumuuza, watanipa majibu kuanzia kesho (leo Jumamosi) juu
ya kiasi watakachomuuza ila wapo wazi kwa biashara.”
“Uwezekano upo lakini kwanza tunatakiwa kusubiri
kuona Fifa itaamua nini katika hilo, nilishafungua madai juu ya matatizo
hayo kumbuka Cannes wanaweza kupoteza nafasi yao ya umiliki wa Kapombe
kutokana na tatizo la kutomlipa malipo yake ya msingi,’’ alisema Kadito.
source; mwanaspoti.co.tz
source; mwanaspoti.co.tz
No comments:
Post a Comment