. Mkutano wa Chadema wa kumaliza kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani mjini Arusha, jana ulivunjika baada ya bomu kulipuka na kuua watu wanne na wengine kujeruhiwa.
Bomu hilo lililipuka jana saa 11:50 dakika chache
kabla ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe kumaliza
kuhutubia mkutano huo uliofanyika katika Viwanja vya Soweto mjini Arusha
na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.
Hilo ni tukio la pili la bomu kulipuka katika
mkusanyiko wa watu, Mei 5 mwaka huu bomu lililipuka katika Kanisa
Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit mjini Arusha
na kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru Frida Mokiti alisema katika hospitali yake kuna maiti moja ya mtoto na majeruhi 11.
Habari zingine zilisema katika hospitali ya
Misheni ya Selian kuna maiti za watu wawili, waliokufa kutokana na
shambulio hilo na majeruhi ambao idadi yao haijafahamika.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha, Liberatus Sabas alisema katika tukio hilo watu wawili wamepoteza
maisha, mwanamke na mwanamume na kwamba idadi ya majeruhi bado
haijafahamika kwa kuwa wametawanywa katika hospitali mbalimbali mkoani
humo.
Watu walioshuhudia tukio hilo walikiambia chanzo chetu kuwa bomu hilo lililipuka karibu na jukwaa walilokuwa wamekaa
viongozi wa Chadema, wakati Mbowe na Mbunge wa Arusha mjini Godbless
Lema wakiwa katika hatua za kumaliza kuhutubia.
Taarifa zilidai kuwa kuna mtu alionekana akirusha
kitu kinachodaiwa bomu kwenye eneo la jukwaa karibu na gari la matangazo
la chama hicho, lakini alipokuwa akifuatiliwa baada ya kutokea mlipuko
huo, polisi nao walikuwa wameanza kudhibiti watu kwa kulipua mabomu ya
kutoa machozi na kupiga risasi za moto hali iliyozidisha taharuki.
Baada ya tukio hilo watu waliokuwa katika mkutano
huo walitawanyika wakikimbia kuokoa maisha yao huku wakimwacha Mbowe na
Lema na viongozi wengine wakiwa bado wako jukwaani.
Hali hiyo ilifanya barabara zote za mji wa Arusha kujaa watu waliokuwa wakikimbia ovyo.
Hali hiyo ya watu kukimbia ovyo kuliwafanya askari
polisi wengi kuingia mitaani kudhibiti watu na hivyo nao kulazimika
kutumia mabomu ya machozi hali ambayo ilizidisha taharuki.
Baadhi ya watu waliojeruhiwa walikimbizwa katika
Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na wengine katika Hospitali ya Seliani
na wafuasi wa Chadema na watu wengine waliokuwa katika eneo hilo.
Miongoni mwa watu waliojeruhiwa katika tukio hilo la mlipuko wa
bomu ni Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa ambaye
amelazwa katika hospitali ya Selian.
Mbowe akizungumza katika hospitali ya Selian jana
aliwataka wanachama wa chama hicho watulie kwa sababu tukio hilo ni
kubwa na lina mambo mengi ndani yake.
Alisema wanachofanya sasa ni kuhakikisha kuwa watu waliojeruhiwa katika tukio hilo wanapata matibabu kwanza.
Mbowe aliwataka watu wote waliopotelewa na ndugu kufika katika hospitali zote za mji wa Arusha kutambua ndugu zao waliojeruhiwa.
Alisema Chadema itagharimia matibabu ya watu wote waliojeruhiwa katika tukio hilo.
Mbowe alisema chama chake kwa sasa hakiwezi kutoa
tamko lolote kuhusiana na tukio hilo la bomu kwa sababu wanafuatiliwa na
baadhi ya askari polisi na maofisa wa Usalama wa Taifa.
Katika hospitali ya Selian, Mganga wa zamu, Dk
Ekenywa alisema kuwa hospitali hiyo imepokea majeruhi 25 ambao
wanaendelea kupatiwa matibabu.
Waandishi wa habari walishuhudia baadhi ya
wanachma wa Chadena pamoja na viongozi wao akiwamo Mbowe wakitoa damu
kwa ajili ya majeruhi.
Awali Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana
alihitimisha kampeni kwa chopa katika Kata ya Makuyuni, wilayani Monduli
na kukumbana na mkutano wa kampeni wa CCM uliokuwa ukihutubiwa na
Mbunge wa Jimbo hilo, Edward Lowassa.
Viongozi hao, walifanya mikutano katika kata hiyo
na kila chama kilitamba kushinda leo na kuwaondoa wananchi na hofu za
kutokea vurugu.
Mbowe licha ya kufanya mkutano huo, pia alifanya
mikutano katika Kata ya Kaloleni Uwanja wa Soweto mjini Arusha na mamia
ya wakazi wa Arusha wa kata zote nne na mkoani Manyara, katika
kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani unaofanyika katika kata
mbalimbali nchini.
Uchaguzi mdogo wa kata nne za Jiji la Arusha na Kata ya Makuyuni, wilayani Monduli, unatarajiwa kufanyika leo.
Uchaguzi wa Kata ya Makuyuni, unafanyika kuziba nafasi ya Diwani
wa CCM, Abdilah Warsama aliyefariki dunia, kata nne za Jiji la Arusha,
uchaguzi unafanyika kutokana na waliokuwa madiwani wa Chadema kufukuzwa
uanachama kwa tuhuma za kukisaliti chama hicho.
Vyama vilivyosimamisha wanaogombea udiwani ni CCM,
Chadema na CUF. Kwa upande wa CCM ni Emanuel Meliali (Kaloleni),
Emmannuel Laizer (Elerai), Edna Jonathan Sauli (Kimandolu) na Victor
Mkolwe (Themi) .
Chadema wanaogombea ni Melance Kinabo “Kaburu”
(Themi), Emmannuel Kessy (Kaloleni), Jeremiah Mpinga (Elerai) na Rayson
Ngowi (Kimandolu).
Kwa upande wa CUF waliosimamishwa kugombea ni Abbas Mkindi Darwesh (Kaloleni) John Bayo (Elerai) na Lobora Ndarvoi (Themi).
Kampeni
Kampeni za uchaguzi huo, mdogo, zilikuwa na
upinzani mkubwa na kwa Jiji la Arusha, wakati Chadema, ilikuwa
ikiongozwa na mbunge wa jimbo hilo, Godbless Lema, CCM iliwatumia vigogo
wake wote wa juu wa chama hicho.
Vigogo hao waliokuwa Arusha ni Naibu Katibu Mkuu,
Mwigulu Nchemba, Katibu wa Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye, Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdalah Bulembo.
Wengine waliokuwa Arusha ni Naibu Waziri wa
Tamisemi, Agrey Mwanri, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano), Stephen
Wassira na wabunge kadhaa wakiongozwa na mbunge wa Simanjiro,
Christopha ole Sendeka.
Kata ya Makuyuni
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole
Nangole alisema jana kuwa chama hicho, kina uhakika wa ushindi katika
Kata ya Makuyuni na kata nne za Arusha.
“Tumefanya kampeni kwa amani na utulivu na nina imani ya ushindi mkubwa hasa hapa Makuyuni,” alisema Nangole.
Mbowe katika kata hiyo, jana alifanya mkutano mfupi baada ya kutua kwa chopa, akitokea mkoani Manyara
Mbowe aliwataka wakazi wa kata hiyo, wasiwe na
hofu wajitokeze kupiga kura leo. Kwa upande wa Lowassa, ambaye ameweka
kambi katika kata hiyo, pia alitoa wito kwa wakazi wa kata hiyo,
kujitokeza kwa wingi kupiga kura leo.
Kwa pamoja viongozi hao ambao walipishana muda
mfupi, Mbowe akianza kupita na baadaye Lowassa kuhitimisha mkutano, kila
mmoja alitamba chama chake kushinda leo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Nape alisema chama hicho kina imani na ushindi leo na alipongeza kampeni kuwa za amani.
“Tuna imani polisi wataimarisha ulinzi leo,” alisema Nape.
Nape jana jioni, alitarajiwa kuhitimisha kampeni mkoani Manyara.
Lema akizungumza katika mikutano jana, alisema wana imani Chadema itaibuka na ushindi katika kata zote.
Wakati huohuo taarifa ambazo blog hii imezipata hivi punde, tume ya Taifa ya uchaguzi imeahirisha uchaguzi uliokuwa ufanyike leo katika kata 4 za jiji la Arusha hadi tarehe 30/06/2013 kutokana na machafuko yaliyotokea jana
Wakati huohuo taarifa ambazo blog hii imezipata hivi punde, tume ya Taifa ya uchaguzi imeahirisha uchaguzi uliokuwa ufanyike leo katika kata 4 za jiji la Arusha hadi tarehe 30/06/2013 kutokana na machafuko yaliyotokea jana
polisi so suluhu ya vurugu kwani baadhi yao hutumiwa na viongzi wa chama tawla kuleta vurugu na mauji
ReplyDelete