MWENYEKITI
wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema pamoja na
kusaini Yanga SC, Mrisho Khalfan Ngassa bado ni mchezaji halali wa
klabu yake na ana makataba wa mwaka mmoja zaidi, aliosaini Agosti mwaka
jana.
Akizungumza
na CHANZO CHETU jana mjini Dar es Salaam, Poppe alisema kwamba hawana
tatizo na mchezaji huyo kuondoka, bali wanataka taratibu zifuatwe na
kwamba tofauti na hivyo suala hilo watalifikisha mbali, ikibidi hadi
FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa).
Akifafanua,
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), alisema
kwamba Simba SC ilizinunua haki zote za mchezaji huyo kutoka Azam ambazo
zilikuwa zinahusu mwaka mmoja na baada ya hapo wakazungumza naye na
kuongeza mwaka mmoja zaidi.
“Ngassa
alisaini Mkataba wa Simba, akaweka saini na dole gumba, tena na tukampa
fedha nzuri tu, kwamba ataichezea Simba SC hadi 2014 Agosti. Na
hatukufanya hivi kienyeji, tulizungumza na Azam FC, wenyewe juu ya
kurefusha mkataba wake, wakatukubalia,”.
“Unajua
nimegundua kitu kimoja, Yanga wana matatizo ya kutojua kanuni, ndiyo
maana mwaka jana walitumia wachezaji ambao wamesimamishwa wakakatwa
pointi. Hili tatizo ni kubwa na lazima walipatie ufumbuzi,”. “Wachukue
muda wao kujifunza sheria, kanuni na taratibu zinazotawala soka,
vinginevyo wataendelea kuwa kichekesho. Eti wanasema sisi tulisaini
mkataba ndani ya mkataba hiyo hairuhusiwi, yaaani wanakariri kariri tu.
“Iko
hivi, klabu hairuhusiwi kusaini mkataba na mchezaji bila kuzungumza na
klabu yake, labda awe amebakiza miezi sita kumaliza mkataba. Sisi
hatukusaini mkataba na Ngassa kienyeji, tulizungumza na klabu yake
kwanza (Azam FC) ikatukubalia, tukazungumza na mchezaji pia akakubali na
akasaini,” alisema Poppe.
Ameongeza
kwamba wanaamini Ngassa ni mtu mzima na mwenye akili timamu na nakala
za mikataba aliyosaini Simba SC tayari zipo TFF, hivyo wanasubiri wakati
ufike wapambane na Yanga kwenye vyombo vya sheria, kwani hawataki
malumbano.
Ngassa
ametambulishwa rasmi asubuhi ya jana makao makuu ya klabu, makutano ya
mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, baada ya kusaini mkataba wa
miaka miwili.
Ngassa
aliichezea Simba SC mechi ya 27 na ya mwisho Jumamosi katika kipindi
cha kuwa kazini Msimbazi, wakati ilala mabao 2-0 mbele ya Yanga.
Siku
hiyo, Ngassa aliwajibika vizuri akiisaidia Simba SC kupata penalti
dakika ya 27, baada ya kuangushwa kwenye eneo la hatari na Nadir Haroub
‘Cannavaro’, wakati huo Yanga inaongoza 1-0, lakini Mussa Mudde
akapoteza nafasi ya kuisawazishia timu yake kwa mkwaju wake kuokolewa na
Ally Mustafa ‘Barthez’.
Katika
mechi 27 alizoichezea Simba SC, zikiwemo za Ligi ya Mabingwa mbili,
kirafiki kadhaa na Ligi Kuu, Ngassa amefunga jumla ya mabao saba na
kutoa pasi za mabao 13.
Baada
ya mechi dhidi ya Yanga Jumamosi, mashabiki wa timu ya Jangwani
walimfuata Ngassa na kumvalisha jezi ya timu hiyo, jambo ambalo
liliwakera mashabiki wa Simba SC.
Ngassa
alitua Simba SC kwa mkopo Agosti mwaka jana akitokea Azam FC ya Dar es
Salaam pia, ambayo nayo iliamua kumtoa kundini baada ya kukerwa na
‘Uyanga wake’.
Ngassa
alifunga bao la pili na la ushindi dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dakika za lala salama katika Nusu Fainali ya
Kombe la Kagame Uwanja Taifa, Dar es Salaam na kwenda kushangilia kwa
kuibusu jezi ya Yanga, jambo ambalo liliwakera Azam na wakatangaza
kumuuza.
Hata
hivyo, Simba SC ilifanikiwa kuipiku Yanga SC kwa kuuziwa mchezaji huyo
kwa Sh. Milioni 25 kwa mkopo. Lakini alipotua Simba SC, ikaelezwa
aliongeza mkataba wa mwaka mmoja na kupewa Sh. Milioni 30, kati ya hizo
Milioni 12 fedha taslimu na Milioni 18, thamani ya gari aina ya Verosa.
Lakini Ngassa mwenyewe alisema alipewa Milioni hizo 30 ili akubali kushuka Msimbazi na si kusaini mkataba mpya.
Ngassa
alisajiliwa Azam Mei 21, mwaka 2010, kwa dola za Kimarekani 40,000,
zaidi ya Sh. Milioni 60 kutoka Yanga SC, huku yeye mwenyewe akipewa dola
30,000, zaidi ya Sh. Milioni 45.
Alitua Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 2006, akitokea Kagera Sugar ya Bukoba, ambayo ilimtoa Toto African ya Mwanza.
Aprili
mwaka 2009, Ngassa alifanya majaribio katika klabu ya West Ham United
ya England wakati huo ipo chini ya kocha Mtaliano, Gianfranco Zola,
ambako pamoja na kuvutia lakini akaambiwa ‘lishe ndogo’.
Aliwahi
pia kufanya majaribio Seattle Sounders FC ya Marekani na akapewa nafasi
ya kucheza kwa dakika nane akitokea benchi kwenye mchezo wa kirafiki
dhidi ya Manchester United na siku hiyo alikaribia kufunga pamoja na
kumuumiza beki Rio Ferdinand.

No comments:
Post a Comment