Kuchaguliwa kwa Lowassa kuongoza kamati hiyo
kunaibua upya vita kati yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, kutokana na wote kutajwa kutaka kugombea
urais katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Awali, Lowassa alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, ambayo iligawanywa hivi karibuni na
kuzaliwa kamati mbili; ya Ulinzi na Usalama na Kamati ya Mambo ya Nje.
Kushinda kwa Lowassa kunakuja siku moja, baada ya
wabunge wote wa CCM kukutana katika kikao cha ndani kilichofanyika
Ukumbi wa Karimjee na kujadili masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na
jinsi ya kuwachagua wenyeviti na makamu wa kamati hizo.
Habari za ndani kutoka katika kikao hicho
zilieleza kuwa moja ya ajenda zilizozungumzwa ni kuwataka wabunge
kuwachagua wenyeviti kwa kufuata taratibu na utendaji wao wa kazi.
Hata hivyo, Naibu Spika Job Ndugai aliliambia
Mwananchi Jumamosi kwamba kikao hicho ni cha kawaida na walikuwa
wakijadiliana matatizo yaliyopo katika majimbo yao na jinsi ya
kuyawasilisha serikalini.
Katika uchaguzi huo, Musa Azzan Zungu ambaye
alikuwa makamu wa Lowassa kabla ya kugawanya kwa kamati hiyo,
amechaguliwa tena kushika nafasi hiyo.
Uchaguzi wa wenyeviti na makamu wao ulifanyika
jana katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku
moja baada ya ofisi ya Bunge kutaja majina ya kamati mpya 16 pamoja na
wajumbe wake.
Uchaguzi huo umefanyika ukiwa umepita mwezi mmoja
tangu kumalizika kwa mkutano wa 10 wa Bunge ambapo, Spika wa Bunge, Anne
Makinda alitangaza mabadiliko ya kamati hizo, huku akiifuta Kamati ya
Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
.
.
Kutokana na mabadiliko hayo, shughuli za POAC sasa zitafanywa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kamati nyingine iliyofutwa ni ile ya Sheria Ndogo
wakati zimeundwa kamati mpya za Bajeti, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa na ya Ulinzi na Usalama.
Taarifa za ndani kutoka katika chaguzi hizo
zinaeleza kuwa Zitto ambaye alikuwa akichuana na John Cheyo, alipata
kura 13 kati ya 17 zilizopigwa na wajumbe wa kamati yake, hivyo Zitto
sasa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
SOURCE.GAZETI LA MWANANCHI
SOURCE.GAZETI LA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment