SERIKALI inatarajia kuajiri walimu 25,000 wa sekondari mwakani ili
kupunguza uhaba wa walimu katika shule za sekondari za Serikali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) Stephen Wasira,
alisema hayo juzi wakati akihutubia mikutano ya hadhara aliyoifanya kwa
nyakati tofauti wilayani humu.
Wasira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda alisema Serikali inatambua
changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu nchini ikiwemo
upungufu wa walimu ambao sasa umegeuka kuwa mzigo kwa wazazi na walezi
ambao wanachanga fedha za kuwalipia mishahara walimu wa kujitolea
wanaofundisha shule hizo.
Alisema mbali na kuwapunguzia mzigo huo wazazi, Serikali pia
itaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa shule
hizo ikiwa ni pamoja na kujenga hosteli na kuweka huduma za maji na
umeme hasa kwa shule za vijijini ili walimu na wanafunzi wapate huduma
hizo kwa urahisi.
“Tutaongeza walimu na kuboresha mazingira ya elimu. Januari mwakani
walimu 25,000 wa Shule za Sekondari wataajiriwa na kupunguza kwa kiasi
kikubwa uhaba wa walimu mashuleni,” alisema Wasira.
Kuhusu madai mbalimbali ya walimu, Wasira alisema Serikali
inayatambua na kuyafanyia kazi kwa kuwa ni watu muhimu katika kuboresha
elimu nchini.
Alikiri kwamba Serikali ilichelewa kuyatatua baadhi ya madai hayo
kutokana na kukabiliwa na hali ngumu ya uchumi na kusema hata hivyo
inaendelea kuyatatua kadiri hali inaporuhusu.
Katika hatua nyingine, Wasira aliwasisitizia umuhimu wa wazazi na
walezi kuwasomesha watoto wao bila ubaguzi akisema elimu haina mbadala
maishani huku akiwataka wajenge uhusiano mzuri na walimu katika
kufuatilia na kusimamia maendeleo ya watoto wao na kukuza taaluma ya
mtoto.
No comments:
Post a Comment