Majina ya wachezaji watano wanaowania tuzo la BBC la mchezaji bora zaidi barani Afrika mwaka 2012 yametangazwa.
Yaya Toure, kwa mwaka wa pili mfululizo, yupo kwenye orodha hiyo.Mwenzake katika timu ya taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba pia yumo.
Wachezaji wengine ni pamoja na Demba Ba kutoka Senegal, Younes Belhanda wa Morocco na nahodha wa timu ya Zambia, Christopher Katongo.
Huu umekuwa ni mwaka wa ufanisi kwa wachezaji hao, na timu za wachezaji wanne zikionyesha ustadi kwa kupata vikombe.
Inaelekea Drogba aliondoka Chelsea wakati muwafaka, mara tu baada ya timu yake kukamilisha msimu kwa ushindi wa klabu bingwa barani Ulaya, hii ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya klabu, na vile vile akipata bao la ushindi katika fainali ya Kombe la FA.
Raia mwenzake wa Ivory Coast, Toure, naye akiichezea Manchester City, aliihakikishia timu yake ubingwa wa ligi kuu ya Premier kwa mara ya kwanza; kombe lao muhimu zaidi katika kipindi cha miaka 44.
Belhanda aliisaidia timu yake ya Ufaransa ya Montpellier kupata ushindi katika ligi ya Ufaransa daraja la kwanza, kwa kufanikiwa kupata magoli 12 katika msimu.
Katika mapambano ya kimataifa, Katongo, kutoka Zambia, naye akiiongoza timu kama nahodha, alifanikiwa kuiwezesha timu yake ya Chipolopolo kuishinda Ivory Coast, na kuibuka mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya kuishinda Ivory Coast katika fainali, kupitia mikwaju ya penalti.
Ba hakung'ara katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya Senegal kuondolewa katika hatua ya makundi, lakini binafsi aliweza kuifanyia timu yake ya Newcastle kazi nzuri, na msimu uliopita alitangazwa kuwa mshambulizi bora zaidi, kwa kufunga jumla ya magoli 17, na kuiwezesha timu kumaliza katika nafasi ya tano.
No comments:
Post a Comment