tuwasiliane

Thursday, November 22, 2012

Chipolopolo kujipima kwa Taifa Stars

MABINGWA Wa Kombe la Mataifa ya Afrika, timu ya taifa ya Zambia(Chipolopolo) nimepanga kuivaa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars)katika pambano la kirafiki la kimataifa litakalofanyika Desemba 23 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana jana kupitia njia ya mtandao ikikikariri Chama cha Soka cha Zambia(FAZ), mchezo huo una lengo la  kuiweka fiti Chipolopolo kabla ya kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika.

Hata hivyo, FAZ haikuweka bayana uwanja utakaotumika kwa ajili ya pambano hilo na badala yake, ilisema utajulikana baada ya majadiliano pande mbili kukamilika.
Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa, baada ya kuivaa Taifa Stars ,Chipolopolo itashuka tena dimba Januari 12 kuikabili timu ya taifa ya Norway katika mtanange utakaopigwa kwenye dimba la Levy Mwanawasa.

"Lengo ni kuhakikisha tunaingia kwenye michuano ya Afrika tukiwa kamili na kutetea ubingwa wetu, mechi dhidi ya Tanzania itaisaidia sana timu ukizingatia wao wamecheza mara nyingi na Ethiopia," ilisema FAZ na kuongeza:
"Hatutachoka, tutaendelea kutafuta mechi zaidi za kujipima nguvu ili kuhakikisha tunafanya vizuri Afrika Kusini,".

Zambia imepangwa kundi C katika michuano ya Mataifa ya Afrika na inazindua kampeni zake kwa kukwaruzana na Ethiopia katika pambano litakalopigwa Januari 21 Uwanja wa Mbombela mjini Nelspruit.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alipotafutwa ili azungumzie taarifa hizo alidai kutofahamu chochote zaidi ya kutaka apewe muda ili kuulizia mamlaka husika.

"Sifahamu chohote kuhusu taarifa hizo, nipe muda niulizie kwa mamlaka husika halafu nitakujulisha," alisema wambua.

Wakati huohuo, mabeki wa timu taifa Kilimanjaro Stars inayojiandaa na michuano ya Chalenji, Kevin Yondan, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe wamesema wamejipanga kuhakikisha wanatwaa taji hilo ugenini nchini Uganda.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kutoka Mwanza ambako timu imepiga kambi, walisema maandalizi yao yanakwenda vizuri na hiyo inawapa matumaini ya kufanya vizuri.
Nyoni alisema kikosi kiko fiti hasa ukizingatia kuwa wachezaji wametoka kwenye michuano ya ligi na kujiunga moja kwa moja na kambi ya timu ya taifa.
"ligi ilikuwa na ushindani mkubwa, hivyo natumani wachezaji wako fiti sambamba na mazoezi tunayopewa," alisema Nyoni.

Kwa upande wake, Yondan alisema: "Ukishaingia kwenye mashindano kinachofuata ni ushindani, na sisi tumejiandaa kushindana kwa mafanikio.
"Tunakwenda kupambana na siyo kusindikiza wengine, dhamira yetu kambini siyo kwenda kuwa ngazi ya wengine kupata mafanikio.

Kapombe alisema atatumia uzoefu wake alioupata kuhakikisha anachezaji wa kujituma na kuwahamasisha wachezaji wenzake kuongeza juhudi ili kurejea nyumbani na kombe.
SOURCE; GAZETI LA MWANANCHI

No comments:

Post a Comment