tuwasiliane

Tuesday, October 30, 2012

Mussa Mudde arejea Simba,

KIUNGO wa timu ya Taifa ya Uganda, Mussa Mudde ametishia uhai wa wachezaji watatu wa kigeni wa Simba baada ya kutamka kuwa yupo fiti.
"Nipo fiti na narudi kikosini Simba katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara."

Tamko la Mudde mwenye mkataba wa miaka miwili na Simba, linakwenda pamoja na kauli ya uongozi ambao umepigilia msumari kwamba wachezaji wake watatu wa kigeni kwa kuwataja kwa majina Paschal Ochieng wa Kenya, Komanbilli Keita wa Mali na Daniel Akuffo wa Ghana wameshindwa kufikia malengo ya klabu hiyo ya Msimbazi.

Mudde aliiambia Mwanaspoti jana Ijumaa kwa simu kutoka Kampala, Uganda kuwa amepona kabisa

"Nipo fiti, nimepona kabisa enka ya kushoto iliyokuwa inanisumbua na nimezungumza na viongozi wa Simba, nitarudi mzunguko wa pili kufanya kazi. "Naweza kucheza na nafanya mazoezi binafsi kwa nguvu na ndiyo maana unaona hata kwenye timu ya Taifa ya Uganda nipo. Kocha anatambua uwezo wangu hataki kunipoteza.

"Bado nina mkataba na Simba wa miaka miwili, hata sijafanya kazi miezi sita," alisisitiza na kudai akiingia kikosini anaweza kucheza nafasi ya ulinzi au kiungo kulingana na matakwa ya kocha Milovan Cirkovic.

Hiyo inahatarisha zaidi ajira ya Keita ambaye hajacheza hata mechi moja ya ligi na uwezekano wa kocha kumtumia tena ni mdogo.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' aliwataja Ochieng, Keita na Akuffo kuwa hawajafikia malengo.

Alisema waliwasajili wachezaji hao baada ya kupitishwa na kocha wao Cirkovic kwa kufanya vizuri katika mazoezi yaliyokuwa yakifanyika katika kambi yao mjini Arusha.

Kaburu alisema: "Si siri wachezaji hao hawajafikia malengo, kuna makosa ambayo mwalimu aliyafanya. Baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, tutapitia ripoti ya kocha kuhusu wachezaji hao pamoja na mwenendo mzima wa ligi."

Hata hivyo, Kaburu alisema Ochieng ameanza kucheza baadhi ya mechi huku Keita akiwa majeruhi kwa muda mrefu jambo linalokuwa gumu kuwahukumu moja kwa moja, lakini ukweli unabaki kuwa wameshindwa kutimiza matakwa ya klabu.

Alisema uongozi umejitahidi kufanya kila kitu kinachotakiwa kufanywa ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara na posho kwa wakati, kuiweka timu kambini pamoja na mambo mengine, lakini timu hiyo imeshindwa kufanya vizuri katika mechi nne za hivi karibuni.

Alishangazwa na sare nne mfululizo ambazo timu hiyo imezipata na kusema zinatokana na uzembe na kushindwa kujituma kwa wachezaji na kocha Milovan kushindwa kuwatumia wachezaji alionao jambo ambalo pia litajadiliwa baada ya mzunguko wa kwanza.

"Mfano alimchezesha Jonas Mkude katika mechi dhidi ya Yanga, kijana alicheza vizuri, lakini mechi dhidi ya Kagera Sugar, mchezaji huyo akaanzia benchi. Tatizo kubwa la Simba ni kiungo mkabaji na nadhani Mkude ni mzuri kwa nafasi hiyo. Mimi nadhani mwalimu anapaswa kuwapa nafasi vijana kama Mkude na wenzake," alisema Kaburu.

Simba itacheza na Azam FC leo Jumamosi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Pambano hilo linatabiriwa kuwa moto wa kuotea mbali.
  

No comments:

Post a Comment