tuwasiliane

Saturday, July 28, 2012

28 JUL.Simba kusajili bonge la beki wa Rwanda


SIMBA inamwania beki kisiki wa APR ya Rwanda, Mbuyu Twite, kwa ajili ya kujiimarisha kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Kiongozi mmoja wa juu wa klabu hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina, aliliambia Mwanaspoti kuwa wamevutiwa na uwezo wa mchezaji huyo na wameanza mazungumzo naye kuhakikisha anaichezea timu hiyo msimu ujao.

"Kila mtu ameona uwezo wake, ana umbo dogo lakini shughuli yake uwanjani imeonekana, ni beki mzuri na nafikiri atatusaidia kuziba pengo la Yondani maana timu yetu sasa hivi ina tatizo kubwa katika nafasi hiyo," alisema.

"Tumeshaanza mazungumzo naye na tunaendelea naamini atakubali, mambo yakiwa mazuri tutaweka wazi kila kitu."

Twite alikiqmbia chanzo chetu kuwa ameshamaliza mkataba na klabu ya APR, kwa hiyo milango iko wazi kwa timu yoyote inayotaka kumsajili, lakini anachoangalia ni maslahi tu.

"Hapa naichezea APR kwa makubaliano, lakini mkataba wangu na timu hii umemalizika tayari. Ila milango iko wazi kwa timu yoyote inayonihitaji, mpira kazi yangu naweza kucheza popote," alisema Twite, ambaye ana pacha wake Kabange Twite aliye naye APR.

Twite ameonyesha soka la kiwango cha juu katika nafasi ya beki wa kati kwenye michuano ya Kagame inayomalizika leo Jumamosi na amekuwa msaada mkubwa kwa APR.

Mchezaji huyo ambaye pia humudu kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, anakumbukwa vizuri na kipa wa Simba, Juma Kaseja. Ndiyo aliyemfunga mabao mawili ya aina moja kutoka umbali wa mita 40 wakati huo Kaseja akiidakia Yanga msimu wa 2008.

Simba inahaha hivi sasa kuimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo ambayo imeonekana kuyumba kwenye michuano hiyo ya Kagame baada ya kuondoka kwa Kelvin Yondani aliyetimkia Yanga.
SOURCE; GAZETI LA MWANASPOTI

No comments:

Post a Comment