


KISASI cha milioni nane! Hivi ndivyo unavyoweza kulielezea pambano la fainali ya Kombe la Kagame baina ya mabingwa watetezi, Yanga dhidi ya Azam FC kuanzia saa 10:00 jioni leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo ambao utatanguliwa na ule wa baina ya Vita ya Congo na APR ya Rwanda kwa ajili ya kusaka mshindi wa tatu, unatarajiwa kuwa mkali na msisimko mkubwa.
Yanga itaingia na hasira ya kutaka kulipa kisasi cha kufungwa mabao 3-1 na Azam kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika Machi 10.
Pamoja na Yanga kutaka kulipa kisasi cha mabao hayo, pia ina uchungu na wachezaji wake kufungiwa na klabu kutakiwa kulipa faini ya Sh milioni nane kutokana na vurugu za mechi ile hivyo kuzidisha hasira za kushinda mchezo huu.
Yanga imeingia fainali baada ya kuifunga APR bao 1-0 wakati Azam imetinga hatua hiyo baada ya kuichapa AS Vita mabao 2-1.
KUKUTANA
Timu hizo zinakutana mara ya tatu mwaka huu, mara ya kwanza zilipambana kwenye Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar mapema Januari na Azam kuibuka na ushindi wa mabao 3- 0.
Kisha zikakutana kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Azam kushinda mabao 3-1.
KISASI
Mchezo huo pia utakuwa wa visasi kutokana na tukio lililotokea kwenye pambano la Machi 10 kwani wachezaji wa Yanga wakiongozwa na beki Stephano Mwasika walimpiga mwamuzi, Israel Nkongo.
Walifanya hivyo baada ya kukasirishwa na kitendo cha mwamuzi huyo kumtoa kwa kadi nyekundu kiungo mchezeshaji, Haruna Niyonzima, katika dakika ya 13 ya mchezo huo. Niyonzima alitolewa baada ya kuzozana na mwamuzi.
Mapema Niyonzima alikuwa na kadi ya njano aliyopewa baada ya kucheza rafu na baadaye kuonyeshwa njano nyingine na hivyo nyekundu kufuata, kitendo hicho kilitafsiriwa na wachezaji wa Yanga kuwa mwamuzi alikuwa anaibeba Azam.
Ndipo ikaanzisha vurugu iliyofanya Nadir Haroub Cannavaro naye atolewe kwa kadi nyekundu.
Kutokana na tukio hilo Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) liliwafungia Mwasika na Jerry Tegete kutocheza mechi zote zilizosalia za ligi na faini ya Sh milioni mbili kwa kila mmoja wao.
Pia ilimfungia beki Cannavaro kutocheza michezo mitatu na faini ya Sh milioni moja huku pia ikiwafungia viungo Nurdin Bakari na Omega Seme kukosa mechi tatu na faini ya Sh milioni moja kila mmoja.
Yanga ina ghadhabu na tukio lile na wametamba lazima washinde ili kukata ngebe za Azam ambao ni maarufu kwa jina la Wana Lamba Lamba.
Azam nao baada ya kuitoa Simba kwenye robo fainali, inaamini itaendeleza rekodi yao ya kuishinda Yanga.
UBORA WA TIMU
TIMU zote zina ubora wa hali ya juu kuanzia ushambuliaji, viungo na hata safu ya ulinzi.
Lakini vita kubwa itakuwa kati ya washambuliaji watatu, John Boko Adebayor wa Azam, Said Bahanuzi na Hamis Kiiza wa Yanga ambao wote wana mabao matano na kila mmoja atataka kuongeza ili kuchukua Kiatu cha Dhahabu na kumzidi mshambulaiji wa AS Vita Etekiama Taddy mwenye mabao sita.
Adebayor ambaye alimtungua kipa Juma Kaseja mabao matatu Hat Trick, anatarajiwa kuongoza maangamizi sambamba na Kipre Tcheche na Mrisho Ngasa ambaye anaweza kuanza.
Katika mchezo uliopita wa nusu fainali dhidi ya AS Vita, Ngassa alipangwa kikosi cha kwanza na kuipeleka timu yake fainali licha ya kuwepo taarifa kuwa haelewani na kocha, Stewart Hall.
Yanga yenyewe itakuwa ikiwategemea washambuliaji wake pacha Bahanuzi na Kiiza ambao wameunda kombinesheni ya hatari katika michuano hiyo na kocha wao amewapa majukumu ya kuhakikisha Azam inalala na kuipa ubingwa tena timu yao.
Lakini kubwa jingine linalosubiriwa ni kuona ubora wa viungo wachezeshaji Niyonzima na Salum Abubakary Sure Boy wa Azam, ambao wamesababisha mjadala mkubwa miongoni mwa washabiki wa soka kuwa nani mkali baina yao.
Wote wamekuwa wakicheza soka la kiwango cha juu katika timu zao na kitendawili hicho kitateguliwa kwa yeyote atakayempoteza mwenzake uwanjani ndiye atakayeibuka mshindi.
Pia sifa kubwa ya timu hizo mbili ni ubora wa safu ya ulinzi hasa beki ya kati kwani wakati Yanga kuna 'Cannavaro' na Kelvin Yondani Vidic, Azam kuna Aggrey Morris na Said Morad.
Hivyo washambuliaji wa timu hizo wanahitaji akili za kiwango cha juu kuhakikisha wanazipenya ngome hizo na kwenda kufunga mabao.
KAULI ZA MAKOCHA
Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet amesema anafurahia ubora wa kikosi chake na jinsi wachezaji wake wanavyocheza soka kwa nidhamu na anaamini watazidi kuwafurahisha mashabiki wao.
"Kila mara nimekuwa nikisema nataka wachezaji wanaojituma na kujitolea uwanjani na nafurahi wachezaji wangu wananielewa na kufuata kile inachotaka na naamini wataendelea mambo mazuri Jumamosi (leo) dhidi ya Azam na kuweza kuibuka na ushindi," alisema.
"Azam ni kati ya timu bora Tanzania, inacheza soka la pasi nyingi lazima tuzibe mianya na tusiwaruhusu watuchezee mpira naamini tutawashinda."
Kocha wa Azam, Stewart Hall alisema anaiheshimu Yanga kutokana na kiwango walichokionyesha katika michuano hii, lakini amewataka waamuzi kuchezesha kwa haki ili mshindi apatikane kihalali.
"Yanga ni timu kubwa na ina wachezaji wa kiwango cha juu, lakini tumejiandaa kuwakabili na tunachoangalia ni kuweka historia mpya Tanzania na hata nje ya Tanzania kwa kutwaa kombe hili," alisema Hall.
ZAWADI
Bingwa wa michuano hiyo ataondoka dola 30,000 (Sh 47.4 milioni), mshindi wa pili atajinyakulia Dola 20,000 (Sh31.6 milioni) na wa tatu atajipatia Dola 10,000 (Sh 15.8 milioni).
No comments:
Post a Comment