
Baada ya kumfunga kipa namba moja wa Simba, Juma Kaseja mabao matatu katika mechi moja ‘hat-trick’, mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco amesema ataendelea kumtungua zaidi kipa huyo.
Kaseja alifungwa mabao hayo katika mechi ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Kagame dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Taifa, Jumanne iliyopita, iliyomalizika kwa Simba kufungwa mabao 3-1.
Hiyo ni mechi ya pili mfululizo kwa Bocco kumfunga Kaseja, mechi ya mwisho ilikuwa ya fainali ya Kombe la Urafiki ambapo akitokea benchi na kufunga kwa kichwa.
Bocco amesema juhudi binafsi na kujituma ndivyo vinamuwezesha kumfunga kipa huyo anayeaminika kuwa bora zaidi nchini kwa sasa.
“Nimekuwa nikimfunga Kaseja kila wakati kutokana na juhudi binafsi na kujituma uwanjani. Natambua majukumu yangu ndani ya uwanja na kufuata maelekezo ninayopewa na kocha wangu, nitaendelea kumfunga Kaseja kila tutakapokutana,” alisema Bocco.
No comments:
Post a Comment