tuwasiliane

Tuesday, June 5, 2012

05 JUN.Simba yawatema Nyosso, Jabu wamshika Uhuru


CALVIN KIWIA
SIMBA imeachana na mabeki wake wawili; Juma Nyosso na Juma Jabu, lakini imemsainisha upya Uhuru Suleiman.

Habari kutoka ndani ya klabu ya Simba, zinasema kuwa kwa pamoja uongozi umekubali kuwatema mabeki hao wawili ambao hata hivyo mikataba yao ilikuwa imekwisha.

Hata hivyo, Uhuru ambaye mkataba wake ulikuwa umekwisha alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Simba Ijumaa iliyopita.

"Napenda ujue kuwa Nyosso na Jabu wapo huru kwani mikataba yao imekwisha na sisi hatuwahitaji tena ila Uhuru Suleiman amesaini mkataba wa miaka miwili," alisema kiongozi mmoja wa Simba.

Kitendo cha Simba kumsajili Paulo Ngalemwa kutoka Ruvu Shooting ya Pwani kimethibitisha kuwa Juma Jabu hana nafasi tena Msimbazi.

Dirisha dogo la usajili Novemba, mwaka jana uongozi wa Simba ulimtoa kwa mkopo Jabu kwenda kukichezea kikosi cha Villa Squad lakini aligoma na baadaye kumrejesha kundini.

Jabu alisema; "Mkataba wangu na Simba kwa sasa umeisha, siwezi kufahamu wana nia gani na mimi kwa sasa, hakuna kiongozi yeyote aliyenipigia simu wala kuongea na mimi kuhusu kusaini mkataba mpya."

Kutua kwa Paulo Ngalemwa kwenye kikosi cha Simba ambaye hucheza nafasi ya beki wa kushoto kama ilivyo kwa Jabu ni wazi nafasi ya Jabu kuendelea kuichezea Simba msimu ujao haipo kwani kuna beki mwingine wa nafasi hiyo, Amir Maftah.

Beki huyo alisema; "Nipo tayari kwa sasa kufanya mazungumzo na klabu yeyote ya Ligi Kuu kwa lengo la kusaini mkataba mpya endapo tu tutaafikiana."

Alisema; "Thamani yangu nafikiri ni siri yangu, siwezi kuweka wazi kwa sasa, nafikiri nitakapopata timu nitaweka wazi tumepatana kwa kiasi gani lakini si kwa sasa." alisisitiza.

Hata hivyo kutokana na tetesi kuwa anawindwa na watani Yanga alikana na kusema hakuna kiongozi wala mwanachama aliyemfuata kumshawishi kujiunga na Yanga kwa msimu ujao.

"Sichagui timu ya kujiunga nayo, wakija na kuafikiana ambayo nayataka sina pingamizi nao, nachoangalia kwa sasa ni maslahi." alisisitiza.

No comments:

Post a Comment