

Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA) na msanii mkongwe wa Hip Hop nchini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, amepania kukonga nyoyo za mashabiki wake watakaohudhuria tamasha la 'USIKU WA SUGU', huku akiahidi kutoa sh milioni 2 kati ya tatu atakazolipwa kwa shoo hiyo kusaidia Mfuko wa Elimu Jimbo la Mbeya.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, katika mkutano wa kuutambulisha ‘Usiku wa Sugu’ utakaofanyika Jumapili Juni 3 kwenye Ukumbi wa Dar Live, ulioko Mbagala Zakheem, Sugu alisema kwa kuwa ni mara ya kwanza kwake kutumbuiza hapo, atahakikisha anaacha gumzo miongoni mwa watakajitokeza.
“Nilianzia maisha Mbagala na nilitokea huko kwenda kumbi za starehe usiku katikati ya jiji (Posta). Jumapili narejea tena huko nikiahidi kufunika kama kawaida ya shoo za Vinega, huku nikipanga kutumia pato binafsi kusaidia Mfuko wa Elimu jimboni kama nilivyoahidi wakati nikiomba kura,” alifichua Sugu.
Katika usiku huo, Sugu atasindikizwa na wasanii Joseph Haule ‘Profesa Jay’, Juma Kassim ‘Sir Nature’, Danny Msimamo na Maujanja Supplies, huku Sugu mwenyewe akiongeza kuwa mkali wa aina hiyo ya muziki Fred Maliki ‘Mkoloni’ atakuwapo ukumbini.
No comments:
Post a Comment