tuwasiliane

Wednesday, May 30, 2012

30 MAY.Kiwanja kilichomng'oa Mkulo chazua balaa


SAKATA la uuzwaji wa Kiwanja cha Serikali Namba 10 kilichoko Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL), limechukua sura mpya baada ya mpangaji katika kiwanja hicho, Ameka Traders kugoma makabidhiano baina ya Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC) na mnunuzi huyo.

Tukio hilo lilitokea Ijumaa iliyopita wakati watendaji wa CHC na wawakilishi wa Kampuni ya MeTL walipofika kwenye eneo la kiwanja hicho kwa ajili ya makabidhiano.

Mwakilishi wa Kampuni ya Ameka Traders, Bahati Sisala alisema watu hao walifika kwenye kiwanja hicho kwa ajili ya kufanya makabidhiano lakini waligoma kuwaruhusu kuingia.

“Walifika hapa mapema tu mchana kwa ajili ya kukabidhiana, lakini tulishindwa kufungua mlango kwa sababu hawakuwa na kibali cha kuingia ndani, jambo ambalo liliwafanya waishie nje huku wakijadiliana,” alisema Sisala.

Alisema watu hao waliendelea kuwaomba wafungue mlango, lakini walishindwa badala yake wakaamua kuondoka huku wakipeana taarifa za makabidhiano nje ya jengo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC, Dome Malosha alisema siku hiyo watendaji hao walifika kwenye eneo hilo kwa ajili ya kukamilisha makabidhiano.

“Watendaji walikwenda kwa ajili ya kufanya ‘handover’ ya mali za kampuni, lakini tukikamilisha tutawafahamisha kuhusu suala hilo, kwa sasa niko sehemu mbaya siwezi kuongea lolote,” alisema Malosha.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana jana zilieleza kwamba Malosha aliwapigia simu wapangaji hao wa CHC katika kiwanja hicho na kuwataka waende ofisini kwake kwa ajili ya kupewa notisi ya uhamisho.

Wakati hayo yakiendelea, Kampuni ya MeTL imekanusha kununua kiwanja hicho kiholela na kudai kuwa hawajahusika katika hatua yoyote kuhusu tuhuma hizo.

Kiwanja hicho kinadaiwa kuuzwa kwa Sh2.4bilioni na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo huku akidaiwa kuvunja Bodi ya Wakurugenzi ya CHC jambo ambalo lilisababisha kujiuzulu kwake.

Akizungumzia tukio la kuzuiwa kukabidhiwa kiwanja hicho, mmiliki wa MeTL, Gullam Dewji alisema wapangaji hao walikataa kufungua geti kwa maelezo kwamba hawakuwa na taarifa yao.

Hata hivyo, alisema pamoja na tukio hilo hana wasiwasi kwani kiwanja hicho ni chake na anajua atakabidhiwa siku yoyote.

“Sisi hatuna wasiwasi wowote kwa sababu kiwanja ni chetu na tumefuata taratibu zote,” alisema Gullam na kuonyesha vielelezo vya namna alivyokinunua akisema ununuzi huo ulifanyika kihalali na hakuna sheria na taratibu zilizokiukwa.

Alisema MeTL ilikuwa ikimiliki Kiwanja namba 192 ambacho ili kufika, iliwalazimu kupita ndani ya kiwanja kingine.

Alisema kutokana na hali hiyo walilazimika kununua Kiwanja Na.10 ambacho kipo mkabala na eneo lao ili waweze kuweka barabara itakayowawezesha kwenda katika jengo lao.

“Wakati hatua hizo zikifanyika waliokuwa wakitumia kiwanja hicho walikwenda mahakamani na kupewa amri ya Mahakama (Court Injuction) tangu mwaka 1997,” alisema Gullam.

Alisema kuwa pamoja na hali hiyo wao waliiomba CHC wanunue kiwanja hicho Na 10 akisema hata sheria za ununuzi zinaeleza wazi kwamba jambo hilo linawezekana kufanyika.

“Sheria zinaeleza wazi na iwapo kesi ikimaliza, vyovyote itakavyokuwa yanabaki maelewano baina yetu sisi na wale waliokuwa katika hicho kiwanja” alisema Gullam.

Mkulo na Ofisi ya Msajili Hazina waliingia kwenye mvutano na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe baada ya kuituhumu kamati hiyo kuhongwa ili kutetea nyongeza ya muda ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC).

Katika Mkutano wa Nne wa Bunge ambao ulishuhudia mvutano huo bungeni, Zitto aliapa kuwa kama ingebainika alihongwa yeye au wajumbe wake, angejiuzulu na kumtaka Mkulo naye ale kiapo kama hicho ikibainika kuwa maelekezo yake kwenda CHC yalisababisha ufisadi huo, lakini waziri huyo wa zamani aligoma.

Hata hivyo, taarifa ya mwaka huu ya CAG iliyowasilishwa bungeni ilionyesha kuwa Wizara ya Fedha na Ofisi ya Msajili zilihusika moja kwa moja katika uuzaji wa kiwanja hicho.

Sehemu ya ripoti hiyo ya CAG inasema: “Matokeo ya ukaguzi maalumu yalibaini mambo yafuatayo: Ilionekana kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Wizara ya Fedha zilihusika moja kwa moja katika uuzwaji wa Kiwanja Na.10 kilichopo kando ya Barabara ya Nyerere kilichouzwa kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Ltd, bila kuishirikisha Bodi ya Wakurugenzi ya CHC.”

Pia CAG aliitaka Serikali iamue ama kuharakisha kukamilisha ubinafsishaji kwa mashirika yaliyosalia ili kuepusha kuharibika kwa rasilimali zilizopo au ibadilishe uamuzi wake na kuyapa mashirika hayo mtaji yaweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Suala hilo limeshaingia mikononi mwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkurugenzi wake, Dk Edward Hoseah amesema anamchunguza Mkulo kutokana na kashfa hiyo.

SOURCE; www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment