Thursday, April 5, 2012
05 APR. Di Matteo asema wataifunga Barcelona
Meneja wa muda wa Chelsea Roberto di Matteo amesisitiza watakuwa na mpango madhubuti wa kuifunga Barcelona katika mchezo wa nusu fainali ya Ubingwa wa Ulaya
Barcelona itakabiliana na Chelsea ili kutafuta nafasi ya kucheza fainali mwezi wa Mei mjini Munich baada ya Chelsea kuitoa Benfica kwa jumla ya mabao 3-1 kwa ushindi wa mabao 2-1 kwenye pambano la robo fainali uwanja wa Stamford Bridge siku ya Jumatano.
Na Di Matteo anasisitiza Chelsea haiogopi mtazamo wa kukabiliana na mabingwa watetezi wa Ulaya ambao pia wanapewa nafasi kubwa ya kunyakua tena ubingwa huo na kurudiwa kilichotokea katika uwanja wa Stamford Bridge mwaka 2009 wakati wa nusu fainali ambapo bao la dakika za mwisho lililokuwa na utata la Andres Iniesta lililoivusha Barcelona hadi fainali.
Di Matteo alisema: "Litakuwa jambo la faraja kukabiliana na timu bora duniani katika michezo miwili. Tutatafuta mikakati itakayotumiwa na wachezaji wetu na hatimaye kuwafunga Barcelona."
"Itakuwa ni mchanganyiko wa kucheza kwa nguvu zetu zote huku tukitilia maanani ubora wao.
"Bila shaka wana wachezaji wenye vipaji binafsi ambao ni tishio kubwa na ni hatari sana, lakini hatuna budi kucheza mchezo wetu kwa nguvu zetu zote."
Chelsea walihisi hawakuwa na bahati walipochapwa na kikosi cha Pep Guardiola mwaka 2009 na walilalamika vikali kutokana na uamuzi wa mwamuzi kutoka Norway Tom Ovrebo.
Di Matteo aliongeza: "Tumeshakumbana nao mara kadha miaka mingi iliyopita na wachezaji wetu wengi wana kumbukumbu dhidi ya Barcelona na kwa kiasi fulani wanahisi bahati haikuwa upande wao walipopambana nao miaka mitatu iliyopita.
"Itakuwa michezo mizuri yote miwili dhidi yao. Tunasubiri kwa hamu kuwakabili na tuna furaha kubwa kufika hatua hii ya nusu fainali ya Ubingwa wa vilabu vya Ulaya."
Mwalimu wa timu ya Benfica Jorge Jesus alihisi kikosi chake hakikuwa na bahati ya kusonga mbele.
Alisema: "Tulicheza vizuri sana Lisbon na London. Najivunia wachezaji wangu.
"Tulicheza tukiwa 10 kwa muda wa saa nzima na bado tulikuwa wazuri. Tuliwafanya Chelsea waonekane ni timu ya kawaida tu."
Jambo moja ambalo halikuwa zuri kwa Chelsea ni kuumia kwa nahodha wao John Terry.
Mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 31 alitolewa na nafasi yake ikachukuliwa na Gary Cahill katika dakika ya 59.
"Aligongwa mbavuni na ndio sababu iliyotufanya tumtoe," Di Matteo alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment