Friday, April 6, 2012
06 APR. Kila la heri Simba leo
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania waliobakia kwenye michuano ya kimataifa ngazi ya klabu,
timu ya Simba leo inashuka dimbani nchini Algeria kupambana na timu ya ES Setif huko kwenye mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza Kombe la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).
Kwenye mchezo wa awali uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Emmanuel Okwi na Haruna Moshi.
Kutokana na matokeo hayo kwenye mchezo huo wa ugenini Simba itahitaji sare ama ushindi wa aina yoyote ili isonge mbele huku timu hiyo ya Algeria ikihitaji zaidi ya ushindi wa kuanzia mabao 3-0 kusonga mbele.
Simba imekuwa ikizipa usumbufu timu za ukanda wa nchi za Kiarabu na mara nyingi imekuwa ikishinda nyumbani, ingawa ugenini haifanyi vizuri sana, lakini wakati mwingine hata ugenini imekuwa ikifanya maajabu.
Itaingia uwanjani leo ikiwa na kumbukumbu ya mwaka 1993 katika robo fainali ya Kombe la CAF, ambapo Simba iliifunga USM El Harrach ya Algeria mabao 3-0 Uwanja wa Uhuru
wakati huo ukiitwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na zilipoenda kurudiana Algeria Simba ikalala mabao 2-0, lakini ikasonga mbele.
Mwaka 1974 Simba iliifunga Mehlala ya Misri bao 1-0 jijini Dar es Salaam. Timu nyingine zilizowahi kufungwa na Simba ni JET ya Algeria, Zamalek ya Misri ambayo ilivuliwa ubingwa wa Afrika mwaka 2003.
Ilifungwa Dar es Salaam bao 1-0 nayo ikaenda kushinda Cairo, Misri bao 1-0, zikapigiana penalti Simba ikashinda 3-2.
Waarabu wengine waliowahi kuonja kipigo cha Simba ni Al Ahly ya Misri, ambayo ilifungwa mabao 2-1 Tanzania na ikashinda mabao 2-0 kwao mwaka 1985 na wengine ni Al Mokaoulun ya Misri ilifungwa Dar es Salaam mabao 3-1 ikashinda kwao mabao 2-0.
Mwaka juzi Simba iliinyuka Haras El Hodoud ya Misri mabao 2-1 na ikaenda kufungwa Alexandria mabao 5-1. Yote ni michuano inayoandaliwa na CAF kwa ngazi ya klabu.
Simba ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania waliobaki katika michuano inayoandaliwa na CAF kwa ngazi ya klabu, ambapo wawakilishi wengine wa Tanzania ambao tayari wameshatolewa ni Yanga iliyotolewa na Zamalek ya Misri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Mafunzo iliyokuwa ikicheza Ligi ya Mabingwa Afrika na kutupwa nje na Maqulmano ya Msumbiji.
Nayo Jamhuri ya Pemba ilitolewa michuano ya Kombe la Shirikisho na Hwangwe FC ya Zimbabwe.
Ingawa timu hiyo itakuwa ugenini ni wazi mchezo utakuwa mgumu hivyo benchi la ufundi la timu hiyo chini kocha Milovan Cirkovic linapaswa kucheza mchezo huo kwa tahadhari kubwa na kutoruhusu bao la mapema litakalowapa nguvu Waarabu hao.
Milovan ametamba timu yake kucheza kwa kushambulia na kutafuta walau bao moja ugenini litakalowaweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Maneno ya kocha huyo yaliungwa mkono karibu na wachezaji wote wa timu hiyo wakiongozwa na nahodha Juma Kaseja na washambuliaji Emmanuel Okwi na Felix Sunzu, ambao pia waliahidi kupigana kufa ama kupona kuivusha timu hiyo kwa raundi inayofuata.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage amekaririwa akisema Algeria kuna hali ya hewa ya ubaridi, lakini vijana wapo tayari kwa mchezo huo, hivyo ni jukumu la Watanzania kuwaombea dua ili
waweze kufanya vizuri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment