Thursday, April 5, 2012
05 APR.Chelsea haitakutana na Barcelona
Kocha wa Real Madrid ya Uhispania, Jose Mourinho, amesema hatazamii kukutana na klabu yake ya zamani, Chelsea, katika fainali ya klabu bingwa barani Ulaya.
Real itakutana na Bayern Munich ya Ujerumani katika nusu fainali, baada ya kuishinda Apoel Nicosia, nayo Chelsea itacheza na Barcelona.
Tarehe 17 Aprili, Bayern Munich itacheza na Real Madrid, na tarehe 18 Aprili, Chelsea itacheza na Barcelona.
Tarehe 24 Aprili, Barcelona itacheza na Chelsea, na 25 Aprili Real Madrid imepangwa kucheza na Bayern Munich.
Lakini Mourinho, ambaye amelalamika kwamba inaelekea maafisa wa soka wanaipendelea Barcelona, amesema hatazamii kukutana na The Blues (jina la utani la Chelsea).
"Inaweza kuwa Bayern au Barcelona, lakini sidhani itakuwa ni Real Madrid na Chelsea, na tunajua ni kwa nini", alisema.
"Barcelona sio tu wanatazamiwa kufuzu, bali wanatazamiwa sana kufuzu", aliongezea.
Real wamewahi kuwashinda wapinzani wao wa Uhispania mara moja tu, baada ya kukutana mara kumi tangu Mourinho aanze kuifundisha klabu hiyo ya Bernabeu alipoondoka Milan mwaka 2010.
Mourinho ameshawahi kunukuliwa akisema ni jambo "lisilowezekana" kupata ushindi katika uwanja wa Barcelona wa Nou Camp, na amekuwa akigombana na klabu hiyo tangu nyakati za zamani akiifundisha Chelsea.
Kuhusiana na kukutana na Bayern Munich, Mourinho alisema: "Bayern ni klabu kikali mno".
"Ni timu ambayo ninaifahamu vyema, na haijabadilika mno na timu niliyocheza nayo kombe la klabu bingwa nikiifundisha Inter Milan miaka miwili iliyopita, na wana wachezaji hodari ambao kibinafsi ni stadi".
Mourinho, kutokal Ureno, pia alielezea nia yake ya kuendelea kubaki Madrid baada ya msimu huu, na kupuuza uvumi kwamba ana mipango ya kujiunga na Manchester City.
"Kuna mtu aliyesema nimetia saini mkataba na Man City na huo ni uwongo mtupu, na kwa hiyo sifurahi kusikia habari ambazo hazina chembe ya ukweli", alisisitiza.
"Mkataba wangu una miaka miwili zaidi na Madrid. Kila mtu anajua ninaipenda England na siku moja nitarudi huko, lakini hakuna anayefahamu siku nitakayofanya hiyo. Lakini hakuna ukweli wowote kuhusiana na City ama klabu chochote kile".
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment