

WASANII wa muziki wa Hip Hop, E m m a n u e l Simwinga ‘Izzo Business’ na Ibrahim Mussa ‘Roma’, wanatarajia kumaliza uhasama wao katika onesho litakalofanyika Jumapili kwenye Ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala Zakheem, Dar es Salaam.
Uhasama huo ulianza kushika kasi Machi 11 mwaka huu kwenye ukumbi huo, baada ya Izzo kupanda jukwaani kwenye Tamasha la Mnanda dhidi ya Mduara ambapo msanii huyo
alimponda Roma kuwa ni mtoto mdogo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Meneja Matukio wa Dar Live, Abdallah Mrisho ‘Abby Cool’ alisema wasanii hao watapanda jukwaani kumaliza ubishi kati
yao ambapo mashabiki wataweza kuamua nani mkali kati yao.
“Hii ni burudani maalumu na bila shaka mashabiki watakaojitokeza wataweza kufahamu nani mkali kati yao, kwa muda mrefu sasa wamekuwa katika uhasama, lakini Jumapili tutajua
mkali ni nani kati ya Izzo B na Roma, lengo letu sisi ni kuona muziki wa Kizazi unakua na faida katika jamii,” alisema Mrisho.
Alisema licha ya burudani hiyo kutoka kwa wakali hao, pia onesho hilo litasindikizwa na kundi la muziki wa Taarabu la Jahazi Modern, Mashauzi Classic, bendi ya muziki wa dansi ya Akudo Impact na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Kassim Mganga.
Kwa upande wake Izzo akizungumzia onesho hilo, alisema kwa ufupi kwamba wataonyeshana
kazi Jumapili na yeye hapendi kuzungumza maneno mengi.
“Tutaoneshana Jumapili kati yetu nani mkali, mwisho wake au kiama chake kitajulikana kwenye onesho hilo,” alisema Izzo.
Naye Roma akizungumzia onesho hilo alisema alisikia jinsi Izzo alivyofanya na kama yeye alianza yeye atakwenda kumaliza Jumapili.
“Kama yeye (Izzo) alianza kulifungua Dar Live, mimi nitaenda kulifunga hiyo Jumapili na kujua nani mkali kati yetu,” alisema Roma.
No comments:
Post a Comment