tuwasiliane

Tuesday, March 27, 2012

27 MARCH. SIMBA KUWEKA KAMBI CAIRO


Simba wanatarajiwa kuweka kambi mjini Cairo, Misri kwa ajili ya mchezo wa marudiano uliopangwa kufanyika Aprili 6, mjini Setif.
Afisa Habari wa klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga alisema jana kuwa maandalizi ya safari hiyo yameanza kufanyika na wanatarajia kuondoka Jumatatu ijayo.

Kamwaga alisema wameamua kuweka kambi mjini Cairo ili kuzoea hali ya hewa ya huko ambayo inafanana na ile ya mji wa Setif. Alisema lengo la kwenda mapema ni kufanya vyema katika mchezo huo ambao wao wanahitaji ushindi au sare aina yoyote.

Alisema kuwa wamejipanga vilivyo ili kuona kuwa wanafanya vyema katika mchezo ambao wanaamini utakuwa na ushindani wa aina yake.

“Tunakabiliwa na mechi ngumu ya marudiano, lazima tufanye maandalizi ya kina na kisasa zaidi na lazima tuchukue tahadhari mapema,” alisema Kamwaga.

Alisema wanajua ES Setif watajiandaa zaidi ili kuweza kufanya vyema katika mechi hiyo ambayo wao watakuwa wanahitaji ushindi wa mabao 3-0 ili kuweza kufuzu hatua inayofuata.

Alifafanua kuwa wanahitaji kuwa makini zaidi katika mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa wa ‘kisasi’ kutokana na matokeo ya mechi ya kwanza.

Mshindi kati ya mechi hiyo, atacheza na mshindi kati ya mechi ya Al Ahly Shandy ya Sudan na Ferroviario De Maputo ya Msumbiji ambazo zilicheza Jumamosi mjini Maputo na Al Ahly kushinda 1-0.

Wakati huo huo, Jumla ya Sh268milioni zimepatikana katika mchezo huo uliofanyika Jumapili kwenye uUwanja wa Taifa kutokana na watazamaji 41,000 kuhudhuria.

Baada ya makato, Simba imeweka mfukoni Sh127milioni. Kutangazwa kwa mapato hayo mapema kumetokana na teknologia mpya ilioanzishwa na kampuni ya Prime Time Promotions inayoratibu na kusimamia mechi mbalimbali nchini. Prime Time Promotion imeanzisha mfumo wa tiketi wa kisasa 'Electronic tickets'.

No comments:

Post a Comment