tuwasiliane

Monday, March 26, 2012

26 MARCH.Cancer yawanyemelea wanaokuza WOWOWO!


Wanawake wanaotumia dawa za kuongeza makalio na viungo vingine vya mwili wametahadharishwa kuwa wanaweza kupata ugonjwa wa saratani (Cancer).

Aidha, wanawake wanaotumia mashine kutaka kusimamisha matiti wametahadharishwa huenda wakashindwa kunyonyesha watoto baadaye, wakati wanaotumia vifaa maalumu kuridhisha hamu zao za kimapenzi wameelezwa kuwa wataathirika kisaikolojia.

Daktari Ali Mzige katika mahojiano maalumu yaliyozaa habari hii, alisema anashangazwa na wanawake na mabinti wa Kitanzania wanaohangaika kunywa dawa na kuchoma sindano kwa lengo la kuongeza makalio au sehemu zingine za viungo vya miili yao huku wakihatarisha afya zao, ikiwa ni pamoja na kupata saratani bila kujua.

Mzige alisema wako wanawake wengine wanatumia vifaa maalumu ili kujiridhisha kimapenzi na kwamba wanaotumia vifaa hivyo huathirika kisaikolojia bila kufahamu na ndio hao baadaye wanakataa hata kuolewa kwa sababu tayari wameathirika.

“Wanawake hawafahamu wanaiga tu, huko Ulaya wanaofanya mambo haya ya ajabu ni waathirika wa dawa za kulevya au tayari unakuta wameathirika kisaikolojia, lakini sisi tunataka kuiga tu kila kitu badala ya kutumia vitu vya asili,” alisema.

Dk. Mzige ambaye pia ni Mkurugenzi wa Hospitali ya IMTU, alisema haoni makalio makubwa yanawapa faida gani wanawake na kwamba uvutaji wa matiti una husisha uvutaji wa misuli inayoshikilia nyama za matiti na matokeo yake baadaye mhusika anakuja kushindwa kunyonyesha mtoto.

“Wanawake msidanganyike na vidonge, sindano mnaweza kupata saratani. Hivi ukirefusha matiti, maziwa yatoka wapi ukitaka kunyonyesha, acheni kuharibu afya zenu bila sababu,” alisema.

Aliwataka wanawake kuacha kufanya mambo hayo kwa ajili ya kuridhisha watu wengine na kuharibu asili ya mwanamke wa Kitanzania.

“Haya mambo ya kutaka urembo kupita kiasi ndio yalisababisha mke wa Rais wa zamani wa Nigeria, Olesegun Obasanjo,Stella kufa hivi hivi akitafuta urembo wa bandia…unajiuliza
mama kama huyu alikuwa na kila kitu amekwenda kufanya nini, ndio hayo ninayoeleza anakuwa tayari ameathirika kisaikolojia,” alisema.

Mke wa Obasanjo alikufa wakati akifanyiwa operesheni nchini Hispania akipunguza unene.

No comments:

Post a Comment