tuwasiliane

Wednesday, March 21, 2012

21 MARCH.ES Setif ya Algeria kutua alfajiri hii


TIMU ya soka ya ES Setif ya Algeria imetaja majina ya wachezaji 20 itakaotua nao Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa kikosi cha watu 35 cha timu hiyo kinatarajiwa kuwasili saa 12 alfajiri kwa ajili ya mechi ya Kombe la
Shirikisho dhidi ya Simba itakayochezwa Machi 25 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Msafara huo una wachezaji, benchi la ufundi, viongozi wa timu, kiongozi wa msafara kutoka
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Algeria (FAF) wakati watatu ni waandishi wa habari.

“Wachezaji 20 katika msafara huo ni Mohamed Benhamou, Sofiane Bengorine, Riadh
Benchadi, Smain Diss, Farouk Belkaid, Khaled Gourmi, Mourad Delhoum, Said Arroussi, Mokhtar Benmoussa, Tarek Berguiga, Mohamed Aoudi na Amir Karaoui.

“Wengine ni Mohamed El Amine Tiouli, Racid Ferrahi, Youcef Ghezzali, Youssef Sofiane,
Mokhtar Megueni, Rachid Nadji, Abderrahmane Hachoud na Akram Djahnit.

Kocha wa timu hiyo ni Alain Norbert Geiger ambaye ni raia wa Uswisi, “alisema Wambura.

Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda ambao ni Hudu Munyemana
atakayepuliza filimbi, wakati wasaidizi wake ni Felicien Kabanda, Theogene Ndagijimana
na Edouard Bahizi.

Kamishna wa mechi hiyo ni Felix Tangawarima kutoka Zimbabwe.

Iwapo Simba itafanikiwa kusonga mbele itacheza mechi ya kwanza nyumbani Aprili 29 mwaka huu na mshindi kati ya El Ahly Shandy ya Sudan na Ferroviario de Maputo ya Msumbiji ambapo ya marudiano itachezwa kati ya Mei 11, 12 na 13 mwaka huu wakati huohup KOCHA wa Simba, Cirkovic Milovan atalazimika kutafuta mbinu bora haraka ili kuzuia mashambulizi ya hatari ya kipindi cha pili toka timu ya ES Setif ili kujihakikisha matokeo mazuri kwenye mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam.

Udhaifu mkubwa Simba msimu huu upo katika kipindi cha pili, ambapo huonekana kuchoka na kuruhusu mashambulizi mengi langoni mwao jambo lililofanya mpaka sasa kufungwa mabao 9 kati ya 14 katika muda huo.
Rekodi hiyo mbaya ya kiuchezaji iliyoonyeshwa na Simba msimu huu itakuwa ni faida kubwa kwa wapinzani wao ES Setif waliojijengea utamadumi wa kupata ushindi katika kipindi cha pili.

Sifa kubwa waliyonayo ES Setif inayofundishwa na Mswisi Alain Geiger ni kufunga mabao mengi katika kipindi cha pili katika mechi tano walizocheza mashindano mbalimbali nchini Algeria hivi karibuni, ambapo wamefunga mabao 13 katika muda huo.

Safu ya ushambuliaji wa Setif imefunga mabao yake katika dakika za 49, 50, 70, 79 na 90, huo ndiyo muda ambao safu ya ulinzi ya Simba imeruhusu mabao 9 kati ya 14 iliyofungwa msimu huu katika Ligi Kuu na mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Kiyovu.

Matokeo ya ES Setif na wafungaji na muda waliofunga mabao kwenye mabano katika mwezi huu, JSM Bejaia 2 - 3 ES Setif mabao yalifungwa na (Djabou 45, 55 Aoudia 90), ES Setif 4-2 JS Saoura (Djabou (50), Djamai (52), Benmoussa (53), (83), MC El Eulma 1-3 ES Setif ( Benchadi (49), Benmoussa (70), Ferrahi (79), US Tebessa 0-2 ES Setif (Djabou (43), Benmoussa (80).

Mabao waliyofungwa Simba katika kipindi cha pili msimu huu, Kagera 1-1 Simba (Themi Felix (70 Penalti), Toto 3-3 Simba (Toto bao 60),Yanga 1-0 Simba ( Davis Mwape (67), Simba 3-3 Moro United (Mwaikimba(43), Simba 2-1 Coastal Union ( 76 penalti), Simba 3-1 Kagera Sugar (Themi Felix (57), Mtibwa Sugar 1-2 Simba ( Hussein Javu ( 53).

Kombe la Shirikisho, Kiyovu 1-1 Simba (Yusuph Ndayishimiye (87)), Simba 2-1 Kiyovu ( Nelly Mayanja (77).
Ukiangalia rekodi hiyo inaonyesha jinsi gani kocha Milovan anavyohitaji mbinu sahihi zaidi za kiuchezaji hasa kipindi cha pili ili kuizuia Setif yenye safu bora ya ufungaji hasa katika dakika 45 za mwisho.

Wakizungumza baada ya mchezo wao dhidi ya El Eulma, wachezaji wa Setif wanaotegemewa kuongoza mashambulizi dhidi ya Simba, Hachoud Diss, Benmoussa na Benhamou wameisifu ngome yao kwa kucheza vizuri na kuwapa nafasi nzuri ya kutengeneza mashambulizi.

Diss alisema: "Nidhamu yetu ya uchezaji imetusaidia kushinda, naamini tutaendelea hivi hata tutakapocheza Tanzania dhidi ya Simba."

"Tunakubali hatukucheza vizuri kipindi cha kwanza dhidi ya El Eulma, lakini kipindi cha pili tulionyesha uwezo wetu, tunajua mchezo dhidi ya Simba utakuwa tofauti, lakini tunatakiwa kutumia mbinu yetu ya kushambulia kwa umakini na kupata matokeo,"alisema Diss.

Naye Benhamou alisema: "Mabeki wetu wanafanya kazi yao vizuri na kutupa na sisi nafasi ya kuendelea kushambulia kwa haraka na kujiamini."

Benhamou aliungwa mkono na Delhoum ambaye alisema: "Lengo ni mabeki wetu kutoruhusu bao lolote, hivi sasa tupo vizuri."
"Tunatakiwa kuthibitisha ubora huo wakati tutakapocheza ugenini dhidi ya Simba katika kuhakikisha tunapata matokeo mazuri," alisema Delhoum.

Kocha Milovan ni mwenye furaha baada ya kupona kwa wachezaji wake wote majeruhi isipokuwa Juma Jabu.
Daktari wa Simba, Cosmas Kapinga alisema wachezaji wapo katika hali nzuri kiafya na wanaendelea na mazoezi isipokuwa Jabu anayesumbuliwa na majeraha.

Simba na ES Setif zote zimeishafika fainali katika mashindano haya Kombe la Shirikisho la Soka Barani Afrika, ambapo Setif walifika fainali mwaka 2009 na kufungwa kwa penati 3-2 na Stade de Malien iliyotwaa ubingwa.
Katika mechi ya kwanza iliyozikutanisha timu hizo ES Setif iliichapa Stade de Malien 2-0 nchini Algeria na ziliporudiana nchini Mali timu ya Stade de Malien ilishinda 2-0.

Simba walifika fainali katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Barani Afrika mwaka 1993, ambapo ilicheza mechi ya kwanza na Stella Club na kutoka suluhu 0-0 nchini Ivory Coast na zilirudiana nchini Tanzani, timu ya Simba ilifungwa 2-0 na Stella kutwaa ubingwa.

Hata hivyo ES Setif waliwahi kutwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Barani Afrika mwaka 1988.

No comments:

Post a Comment