
CHAMA cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT), kimedai kuwa beki Stephano Mwasika amewasilisha ujumbe kwa chama hicho kumuomba radhi mwamuzi Israel Nkongo.
Mwasika (pichani) alimpiga Nkongo wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga na Azam zaidi ya wiki moja iliyopita na Yanga kufungwa mabao 3-1.
Mchezo uliotawaliwa na vurugu za wachezaji mbalimbali wa Yanga kudaiwa kumshambulia Nkongo aliyechezesha mechi hiyo.
Kutokana na tukio hilo, Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilitoa adhabu kwa wachezaji watano wa Yanga akiwemo Mwasika ambaye amefungiwa mwaka mmoja.
Wengine ni Jerry Tegete aliyefungiwa miezi sita, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyefungiwa mechi sita na Omega Seme na Nurdin Bakari waliofungiwa mechi tatu kila mmoja.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa FRAT, Leslie Liunda alidai Mwasika amekiomba chama hicho kumuombea radhi kwa Nkongo kwa kosa hilo la kumpiga.
Liunda alidai Mwasika alimpigia simu kumuomba awasilishe maombi yake yakutaka kusamehewa na Nkongo hatua ambayo hata hivyo Liunda alisema haitoshi na kwamba anachotakiwa ni kuomba msamaha kwa jamii na kukiri amefanya kosa.
Mwasika hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo. Liunda alikemea vitendo vya kupiga waamuzi na kwamba mambo hayo ni ya miaka ya zamani na kwamba ni aibu kwa Taifa.
Akitoa tamko rasmi la Frat kwa waandishi wa habari kuhusiana na kupigwa kwa mwamuzi huyo, Liunda alisema kuwa chama chake kinakemea vikali kitendo hicho na kutaka kikomeshwe mara moja.
Akijibu swali kuhusiana na malalamiko ya siku za karibuni yakiwahusisha waamuzi na rushwa, alisema hawezi kuthibitisha na kwamba wakati mwingine waamuzi wanashindwa kumudu mchezo kutokana na uwezo mdogo.
Hata hivyo alisema kama kuna klabu ina ushahidi kuhusiana na waamuzi iwasilishe malalamiko yake FRAT au TFF ili yashughulikiwe.
No comments:
Post a Comment