tuwasiliane

Tuesday, March 20, 2012

20 MARCH.Simba nguvu zote kwa Waalgeria

KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic, amesema, wapinzani wao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, timu ya Es Setif ya Algeria ni wazuri kutokana na kuwaona katika michezo mbalimbali kupitia mikanda ya video na kwenye mitandao.

Simba inatarajia kuwakaribisha wapinzani wao hao kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam Jumapili hii. Na wanataraji kuwasili nchini Alhamisi.

Akizungumza mjini hapa baada ya mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar juzi, kocha Milovan alisema alibaini uwezo wa wapinzani wake kupitia mikanda ya video na mitandao mbalimbali na kwamba wamekuwa wakipata ushindi kwenye mechi mbalimbali za kimataifa.

Alisema, kwa hiyo jukumu alilonalo kwa muda huu mchache ni kukakikisha anawapa mazoezi ya kutosha wachezaji wake na mbinu za mchezo ili kuikabili timu hiyo na hatimaye kupata ushindi mnono kwenye uwanja wa nyumbani.

“Michezo ya sasa ya Ligi Kuu ni moja ya kuwajenga kikamilifu wachezaji na kuona kasoro mbalimbali za kuzifanyia kazi kabla ya mchezo wetu na Es Setif , ambayo ni timu kubwa na ina historia nzuri ya kufanya vyema kwenye michezo yake ya ndani na ya kimataifa,” alisema.

“Nimesoma historia ya timu hii na uwezo wao katika mtandao wao, nimegundua ni timu nzuri na ina uwezo mkubwa wameshinda michezo mingi ya kimataifa, hivyo ni jukumu langu kuwanoa zaidi wachezaji wangu,” alisisitiza Milovan.

Kwa mujibu wa Kocha Mkuu huyo, atawapatia mbinu zaidi za kimchezo wachezaji wake ili wazitumie kwa lengo la kupata ushindi katika mchezo huo muhimu kwao.

Simba wanataraji kuingia Kambini leo, wakati beki wake Amir Maftah aliyekosekana katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar kutokana na kusumbuliwa na Malaria anataraji kuanza mazoezi mepesi leo.


Wakati huo huo PAMBANO kati ya Simba na Mtibwa Sugar lililofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri wa mjini hapa juzi, limeingiza Sh milioni 31.2, imeelezwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Morogoro, (MRFA), Hamis Semka, alisema hayo jana mjini hapa kuwa mapato hayo yametokana na watazamaji wapatao 10,410 waliokata tiketi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, kiasi kilichopatikana ni Sh 31,230,000 na katika mgawanyo, kila timu ilipata Sh 6,508,230 wakati gharama za uwanja ni Sh 2,169,410 hali kadhalika na mgawo kama huo kwa Shirikisho la Soka Tanzania ( TFF).

Mbali na hao, pia MRFA imepata mgawo wa Sh 867,764, Mfuko wa Kuendeleza Soka la Vijana Wadogo (FDF) Sh 1,084,705 na BMT Sh 216,000.

No comments:

Post a Comment