Tuesday, March 6, 2012
06 MARCH. Ngorongoro kuivaa Sudan, Serengeti Boys yapangwa na Kenya
TIMU ya soka ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ imepangwa kuchuana na Sudan katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa vijana mwakani.
Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo ya 18 iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), Ngorongoro itaikaribisha Sudan kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Aprili 20 na 22 na kurudiana baada ya wiki mbili Khartoum, Sudan.
Kama Ngorongoro itafanikiwa kushinda mchezo huo itakabiliwa na kibarua kigumu zaidi kwa kucheza na miamba ya soka ya Afrika Magharibi, Nigeria.
Hiyo ni nafasi nyingine kwa Serengeti kujaribu tena kusonga mbele baada ya kutolewa kwenye raundi ya pili ya mashindano hayo na timu ya Taifa ya vijana ya Ivory Coast mwaka 2010.
Pamoja na kuonesha kandanda safi kwenye mashindano hayo, vijana hao waliona matumaini yao ya kufuzu kwa mara ya kwanza kwenye fainali hizo yakiyeyuka kwa kutoka sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa marudiano.
Timu hiyo ilifungwa bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Abidjan, na ilikuwa ikihitaji kushinda mchezo wa marudiano ili isonge mbele, lakini wakajikuta wakiishia njiani kwa kupoteza mchezo huo.
Ngorongoro Heroes, chini ya kocha wake Kim Poulsen, ilianza kampeni za matayarisho ya mashindano hayo ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika mwakani kwa kushiriki fainali za vijana za COSAFA zilizofanyika kati ya Desemba 1 na 10 mwaka jana Gaborone, Botswana.
Wakati safari ya Ngorongoro Heroes kuelekea Algeria ambako kutanyika fainali hizo ikionekana kuiva, wadogo zao timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’, nao wamepangwa kucheza na Kenya kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya kufuzu fainali za chini ya umri wa miaka 17 mwakani.
Ratiba hiyo iliyotolewa na CAF inaonesha kuwa Serengeti Boys watacheza mchezo wao wa kwanza nyumbani kati ya Septemba 7 na 9 na kurudiana Nairobi baada ya wiki mbili. Ikiifunga Kenya timu hiyo itacheza na mchezo wake wa raundi ya pili dhidi ya Misri Oktoba mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment