Tuesday, March 6, 2012
06 MARCH.SIMBA KULIMWA FAINI
KLABU ya Simba ipo hatarini kukumbwa na rungu la Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), kufuatia vurugu zilizotokea kwenye mchezo wao wa marudiano dhidi ya Kiyovu uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Simba ilishinda mabao 2-1, wakati awali mechi ya kwanza iliyochezwa Kigali nchini Rwanda wiki mbili zilizopita matokeo yalikuwa bao 1-1.
Moja ya adhabu ambayo Simba inaweza kukumbana nao ni sawa na ile ya Zamalek ya kufungiwa kucheza mechi zake bila ya mashabiki baada ya wapenzi wake walipofanya vurugu msimu uliopita walipocheza dhidi Club African ya Tunisia.
Katika mechi ya Simba na Kiyovu zilizuka vurugu kubwa kwa mashabiki wa Simba na Yanga kutwangana makonde ikiwa ni pamoja na kung'oa viti kitendo kilicholaani vikali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Tukio hilo la vurugu lilitokea wakati wa mapumziko pale mashabiki wa wanaodaiwa kuwa wa Simba walipokwenda sehemu ambayo hukaa wenzao wa Yanga na kuibua vurugu kubwa.
Ofisa habari wa TFF, Bonifance Wambura aliiambia Mwananchi jana kuwa wanasubiri ripoti ya Msimamizi wa uwanja ili kujua gharama za uharibifu uliofanywa na mashabiki hao na timu husika itabeba gharama.
"Mchezo ule ni wa Simba na Kiyovu, TFF tunalaani kwa nguvu zote kitendo kilichofanywa na mashabiki. Huu siyo uungwana hata kidogo, michezo haina utamaduni wa ushabiki wa aina hii. Tunasubiri ripoti ya wasimamizi wa uwanja kujua gharama za uharibifu," alisema Wambura.
Hata hivyo Wambura alisema ripoti ya Kamisaa wa mchezo itakayotumwa CAF ndiyo itakayotoa hatma ya Simba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment