
WACHEZAJI wa Yanga ya Dar es Salaam ambao hawajalipwa mshahara wao wa miezi miwili
wameanza kulipwa kwa awamu.
Habari zilizopatikana jana kutoka kwa baadhi ya wachezaji hao na kuthibitishwa na Ofisa Habari wa Yanga, Luious Sendeu ni kuwa wameanza kulipwa fedha zao, ingawa si zote.
“Kuna baadhi ya wachezaji tumelipwa leo, lakini hatujalipwa fedha zote ni mshahara wa mwezi mmoja. “Ilikuwa tukatae lakini kwa sababu ya hali ngumu tumekubali, ila mambo bado si mazuri,” alisema mmoja kati ya wachezaji mahiri wa timu hiyo.
Naye mchezaji mwingine alimpongeza Kocha Mkuu wa timu hiyo Kostadin Papic kwa kuwa mkweli na kwamba bila yeye pengine hali ingezidi kuwa mbaya kwao.
“Papic ndiye mkombozi wa wachezaji Yanga, ingawa tumelipwa kidogo, lakini bila yeye hata hichi tusingepata,” alisema mchezaji huyo kwa sharti la kutotajwa jina lake.
Jumatatu wiki hii, Papic alifanya mkutano na waandishi wa habari na kuushutumu uongozi kutokana na hali mbaya ya kifedha inayowakabili wachezaji wake, huku naye akilalamikia
nyumba anayoishi kukatiwa umeme na kukosa huduma ya maji.
Kutokana na hali hiyo alisema imeathiri mazoezi ya timu hiyo jambo ambalo ni la hatari kwa maandalizi ya michuano ya kimataifa, ambapo Yanga itacheza na Zamalek Februari mwakani.
Papic alienda mbali zaidi na kudai viongozi wamekuwa hawampi ushirikiano na kila anapowapigia simu hawapokei.
Lakini akizungumza jana Sendeu alisema suala la mambo ya mshahara uongozi unashughulikia na kwamba wameanza kulipwa hivyo hakuna tatizo.
“Hawajalipwa zote, lakini kiasi fulani tayari wamepokea kwa kuanzia, mambo mengine ukimpata Katibu Mkuu yeye atazungumza, ila ninachokuthibitishia ni kwamba tayari wameanza kulipwa,” alisema Sendeu.
No comments:
Post a Comment