tuwasiliane

Friday, December 30, 2011

30 DEC.SIMBA KUJIBIMA MBAVU LEO

TIMU ya Simba ya Dar es Salaam leo inatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki na Mtibwa Sugar kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

Kutokana na hali hiyo Kocha Mkuu wa timu hiyo, Milovan Cirkovic amewaomba mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi kesho kwenye Uwanja wa Azam Chamazi, ambapo timu yao itakuwa ikicheza mechi hiyo.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga ilieleza kuwa timu yake ipo imara kwa mchezo huo na wana matumaini makubwa watafanya vizuri.

“Pambano hilo litakuwa la mwisho kwa Simba kucheza jijini Dar es Salaam mwaka huu. Pambano hilo pia litakuwa la mwisho kwa Simba kabla haijaenda Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyopangwa kuanza Januari 2 mwakani, “ alisema Kamwaga na kuongeza kuwa Simba itaenda Zanzibar Jumapili.

“Mechi hiyo itakuwa ya kwanza kwa Kocha Mkuu wa Simba, Profesa Milovan Cirkovic, kukaa kwenye benchi la ufundi na kuiongoza timu yake hiyo ambayo ni mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi na mabingwa wa kihistoria wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.

“Profesa Cirkovic ameahidi kwamba kwenye pambano hilo atashusha kikosi kamili cha wachezaji wa Simba ili kubaini ni kwa namna gani wachezaji wake wameyaelewa mafunzo yake.

Nawakaribisha wapenzi na wanachama wa Simba na wapenda soka kwa ujumla waje kwa wingi kuiona Simba ikicheza.

Nimesikia kwamba Uwanja wa Azam ni mzuri na utaendana na aina ya mchezo ambao Simba itakuwa ikiucheza chini yangu. Nataka kuonesha soka la asili la Simba,” alisema Kamwaga akimnukuu kocha huyo.

No comments:

Post a Comment