
RAIS Jakaya Kikwete amezitakia mema timu za Simba na Asante Kotoko ya Ghana katika mchezo wake wa leo uliopangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa wa kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania.
Kikwete alitoa salamu hizo kwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage wakati alipowaalika viongozi mbalimbali kupata nao chakula cha jioni Ikulu juzi katika moja ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru.
Katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Rage alisema Rais Kikwete amesema mchezo huo ni muhimu kwa maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru na utatoa burudani safi kwa wakazi wa jijini na mikoa ya jirani watakaokuja kuona mechi ya kihistoria.
“Jana (juzi) nilialikwa kwenye chakula cha jioni na Rais ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru, alitoa salamu kwa mchezo huu wa kesho (leo) ikiwa ni historia kwa timu hizi mbili kukutana katika tukio muhimu sana,” alisema Rage.
Rage alisema kuwa wamepokea salamu hizo kwa mikono miwili na kuwaahidi mashabiki wa soka kuja kwa wingi kushuhudia mchezo huo.
“Kotoko wanavaa rangi nyekundu na sisi tunavaa rangi nyekundu, hii ni mechi ya kihistoria sana kwetu, ila nawasikitikia wenzetu Yanga kwa kushindwa kuadhimisha miaka 50 kwa mchezo wa kesho (leo), sidhani kama watacheza tena na Kotoko kwani tokea wacheze na Kotoko miaka ya nyuma, hawajacheza tena,” alisema Rage.
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Future Century, Hellen Masanja alisema kuwa maandalizi
ya mchezo huo yamekwishakamilika na wanatarajia kuwa na msisimko mkubwa.
Kabla ya mechi hiyo, timu ya soka ya waandishi wa habari za michezo nchini, Taswa FC itapambana na timu ya soka ya kombaini ya Wanawake ya mkoa wa Dar es Salaam, Mzizima United Queens.
Kocha Mkuu wa Simba, Cirkovic Milovan alisema kuwa atatumia mchezo huo kama sehemu ya kuandaa timu yake kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Bara na maandalizi ya mashindano ya kimataifa.
Milovan alisema kuwa wamejiandaa vizuri na amefarijika kuona Simba inaundwa na wachezaji nyota na wenye umri mdogo.
Kocha Mkuu wa Kotoko, Maxwell Konadu alisema kuwa amekuja na kikosi kikali na watatoa
ushindani mkubwa na kushinda mchezo huo.
“Naijua Simba ni moja ya timu kubwa na yenye historia kubwa hapa Afrika, nitapanga kikosi
changu cha kwanza ili kukamilisha furaha ya kuongoza ligi kuu ya Ghana,” alisema Konadu.
No comments:
Post a Comment