
KOCHA wa Chelsea, Andre Villas-Boas amekiita kipigo cha mabao 2-1 walichopata toka Liverpool kwenye Uwanja wao wa nyumbani, kuwa ni "hatua moja kuelekea kwenye wakati mgumu zaidi".
Villas-Boas anakuwa kocha wa kwanza wa 'Blues' kupoteza mechi mbili mfululizo kwenye Uwanja nyumbani tangu kuondoka kwa kocha Claudio Ranieri.
Beki wa zamani wa Chelsea, Glen Johnson ndiye aliyeizamisha timu hiyo kwa kufunga bao la ushindi kwa Liverpool dakika chache kabla ya kumalizika mchezo na kumpa pointi zote tatu kocha Kenny Dalglish.
Kabla ya mechi hiyo, Villas-Boas alishuhudia kikosi chake kikipoteza mchezo dhidi ya Arsenal kwa kuchapwa mabao 5-3 Uwanja wao wa Stamford Bridge.
Kipigo toka Liverpool kimeiacha Chelsea--mabingwa wa mara tatu England nyuma kwa pointi 12 dhidi ya wanaoongoza msimamo Manchester City.
"Ni pigo kubwa kwetu kwenye Ligi Kuu," alisema Villas-Boas.
"Tuna mechi ya nyumbani dhidi ya Wolves wiki ijayo, kabla ya kupambana na Newcastle, na kisha vinara wa ligi. Ni lazima tucheze na kushinda mechi hizo pamoja na ugumu wake."
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu hatima yake baada ya mwenendo mbaya wa Chelsea, Villas-Boas alisema hana wasiwasi kwani klabu yake inamuamini kwa mipango yake ya muda mrefu.
"Mmiliki wa klabu hakulipa bure mamilioni ya pesa kunitoa Porto kunileta Chelsea, halafu alipe tena gharama za kunifukuza hapa," alisema.
"Si suala la mmiliki kuwa na uvumilivu. Nimesema kwamba tumeandaa mipango kuijenga upya klabu, na klabu imeridhia mpango huo. Tunajenga timu bora ya baadaye.
"Mkazo wetu kwa sasa klabuni ni nini tutafanya baadaye, tuna vipaji vya kutosha kushiriki kwenye mashindano yote. Haya ni matarajiao yetu kwa sasa.
"Hakuna namna ya kukwepa katika kutekeleza mipango yetu. Jukumu letu ni kushinda mataji mengi kadri tuwezavyo, na kwa sasa tuna mashindano manne."
Mpinzani wa Villas-Boas, kocha wa Liverpool, Dalglish alikuwa na furaha baada ya matokeo hayo kwani ni mara ya pili kupata ushindi kwenye Uwanja wa Stamford Bridge mwaka huu baada ya Februari kushinda bao 1-0.
Liverpool wako nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ikiwa sawa kwa pointi na Arsenal, Chelsea na Tottenham ambapo kila mmoja ana pointi 22.
Kocha Dalglish alisema mara baada ya mchezo: “Ni siku nzuri kwetu”.
"Tulicheza vizuri hasa zaidi kipindi cha kwanza, sidhani kama kuna mtu atasema hatukustahili kupata pointi tatu. Ilikuwa siku nzuri kwetu.”
Dalglish alichukua nafasi hiyo pia kumtetea Villas-Boas: “Katika taaluma ya mchezo wa soka, hakuna wa kumlaumu. Simfahamu (Villas-Boas), lakini najua alijenga jina vizuri wakati akiwa na Porto. Sijui atalaumiwa kwa kitu gani, lakini kuna heshima kubwa anapewa katika mchezo wa soka.”
No comments:
Post a Comment